Jul 23, 2024 02:57 UTC
  • IRGC yanasa meli ya 'Togo' ikifanya magendo ya mafuta Ghuba ya Uajemi

Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran (IRGC) limefanikiwa kutwaa meli nyingine ya kigeni ikifanya magendo ya mafuta mengi katika maji ya Ghuba ya Uajemi.

Press TV imeripoti habari hiyo na kueleza kuwa, meli hiyo ya kubebea mafuta ya 'Belt Guse' yenye bendera ya Togo, imenaswa katika mji wa bandari wa Bushehr, ulioko kusini mwa Iran.

Kikosi cha Pili cha Majini cha IRGC kimesema katika taarifa ya jana Jumatatu kuwa, wanajeshi wa SEPAH wametwaa meli hiyo iliyobeba lita milioni 1.5 za mafuta ya wizi kusini mwa maji ya Ghuba ya Uajemi.

IRGC imebainisha kuwa, makomandoo wa Jeshi la SEPAH la Iran wamewatia mbaroni mabaharia 12 wa kigeni waliokuwapo kwenye chombo hicho. Taarifa ya SEPAH imesema, mabaharia waliokamatwa wana uraia wa India na Sri Lanka.

Boti za mwendo kasi za jeshi la IRGC

Iran inakabiliwa na vikwazo vya kidhalimu vya Marekani ambavyo havijawahi kuwekwa dhidi ya nchi yoyote nyingine duniani, lakini pamoja na kuwepo hatua hizo zilizo kinyume cha sheria, Jamhuri ya Kiislamu inaendelea kuwafikishia wateja wake mafuta, sambamba na kukabiliana na wafanya magendo wa mafuta yake.

Marekani ina historia ndefu ya kutekeleza vitendo vya uharamia dhidi ya meli za mafuta za Iran kwa kisingizio kuwa eti meli hizo zinakiuka vikwazo vya Washington dhidi ya Tehran.

Tags