Kani: Iran haina mipaka katika kuimarisha uhusiano na Afrika
(last modified Fri, 09 Aug 2024 07:19:22 GMT )
Aug 09, 2024 07:19 UTC
  • Kani: Iran haina mipaka katika kuimarisha uhusiano na Afrika

Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu haina kikomo wala mipaka katika kuimarisha na kupanua uhusiano wake na nchi za bara Afrika.

Ali Bagheri Kani, Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema hayo katika mkutano wake na Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Somalia, Ahmed Moallim Fiqi, pambizoni mwa kikao dha dharura cha Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC mjini Jeddah, Saudi Arabia.

Huku akiukaribisha mpango wa serikali ya Somalia wa kuweka mazingira ya kurejesha uhusiano kati ya nchi hizo mbili, Kani amesisitiza kuwa: “Tunaamini kuwa nchi za Kiislamu zinapaswa kuimarisha uhusiano wao sambamba na maslahi yao ya pamoja na kukabiliana na maadui wa Uislamu duniani, kwa hivyo hatuoni kikomo katika maendeleo na upanuzi wa uhusiano na nchi za Afrika."

Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Iran amesisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inatilia maanani sana suala la kuimarisha uhusiano wake na nchi za Kiafrika.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Somalia kwa upande wake amesema ameridhishwa na mkutano wake na mwenzake wa Iran, sambamba na kulaani hujuma za Israel dhidi ya ardhi, mamlaka ya kujitawala na uthabiti wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

"Tunaheshimu nafasi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kuunga mkono suala la Palestina na kutetea haki za taifa linalodhulumiwa la Palestina," Moallim Fiqi amesema.

Kadhalika Fiqi ameshukuru uungaji mkono wa Iran katika kurejea utulivu na usalama wa Somalia, akipongeza mchango wa Jamhuri ya Kiislamu katika kukabiliana na zimwi la ugaidi.

Tags