Araqchi: Kuimarisha uhusiano na nchi zote ni sera ya serikali ya Iran
(last modified Thu, 29 Aug 2024 07:45:09 GMT )
Aug 29, 2024 07:45 UTC
  • Araqchi: Kuimarisha uhusiano na nchi zote ni sera ya serikali ya Iran

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema sera ya serikali ya 14 ya Iran ni kupanua uhusiano na nchi zote za dunia hususan nchi za Asia Mashariki.

Sayyid Abbas Araghchi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amezungumza na kubadilishana mawazo na Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Japan Yoko Kamikawa kuhusu kustawisha uhusiano wa pande mbili na ushirikiano wa kikanda. Araqchi na Kamikawa wamebainisha haya katika mazungumzo ya simu.  

Araqchi pia ameashiria jinai za utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza na matukio ya karibuni huko Palestina kama moja ya changamoto kuu kimataifa na kusema, vitendo vya kichochezi vya utawala huo yakiwemo mauaji ya shahidi Ismail Haniyeh, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas mjini Tehran, na hatua za Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni za kueneza vita, ni sababu kuu za kushtadi mivutano katika eneo. 

Shahidi, Ismail Haniyeh 

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameongeza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu imeeleza mara nyingi kuwa, tofauti na utawala wa Kizayuni, haitaki kueneza mivutano na migogoro katika eneo.

Katika mazungumzo hayo ya simu, Yoko Kamikawa Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Japan pia amempongeza Sayyid Abbas Araqchi kwa kuteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran na kusema nchi yake ina hamu ya kustawisha uhusiano wa pande mbili kati ya Tokyo na Tehran, na vilevile kuendelezwa ushirikiano wa kieneo na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.