Iran yakanusha madai ya kuwapa mafunzo askari wa Russia huko Ukraine
(last modified Sat, 31 Aug 2024 11:48:54 GMT )
Aug 31, 2024 11:48 UTC
  • Iran yakanusha madai ya kuwapa mafunzo askari wa Russia huko Ukraine

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amepuuzilia mbali madai kwamba mwanajeshi wa Jamhuri ya Kiislamu amekuwa akitoa mafunzo kwa wanajeshi wa Russia katika ardhi ya Ukraine.

Nasser Kan'ani amekanusha madai hayo yasiyo na msingi kwamba afisa wa kijeshi wa Iran alikuwa katika ardhi ya Ukraine kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa vikosi vya Russia.

Amebainisha kuwa Iran haiungi mkono vita akisisitiza haja ya kusimamishwa mgogoro huo na kutatua mizozo kati ya Russia na Ukraine kwa njia ya amani. Kan’ani amebainisha kuwa, kinachoshuhudia nchini Ukraine ni matokeo ya sera na vitendo vya kichochezi vya Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi NATO zikiongozwa na Marekani.

Kauli yake imekuja baada ya mwendesha mashtaka mkuu wa Ukraine kusema kuwa, kesi imefunguliwa dhidi ya jenerali wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) kwa tuhuma za kuisaidia Russia katika uhalifu wa kivita dhidi ya Ukraine.

Kabla ya hapo, Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran alisema kuwa, madai ya Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi NATO kwamba Iran inaisadia kijeshi Russia katika vita vya Ukraine hayana msingi wowote.

Alieleza bayana kwamba, "Kama tulivyokwisha sema mara nyingi, jaribio lolote la kuhusisha vita vya Ukraine na ushirikiano wa pande mbili kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Russia, linafanywa kwa malengo ya kisiasa kwa shabaha ya kuhalalisha uingiliaji kati na kuendeleza misaada ya silaha za Magharibi kwa Ukraine."

Tags