Muirani Mehrzad, mwanaume wa pili kwa urefu zaidi duniani, analala sakafuni katika Kijiji cha Olimpiki, Paris
(last modified Thu, 05 Sep 2024 10:40:47 GMT )
Sep 05, 2024 10:40 UTC
  • Morteza Mehrzad Selakjani
    Morteza Mehrzad Selakjani

Mwanaume wa pili kwa urefu zaidi duniani, Morteza Mehrzad Selakjani ambaye ni raia wa Iran, analazimika kulala chini sakafuni katika Kijiji cha Olympic mjini Paris anakoshiriki michuano ya Olimpiki ya Walemavu inayoendelea sasa nchini Ufaransa.

Michezo ya Olimpiki ya Walemavu (paralympic) inayowashirikisha mamia ya wanariadha wenye mahitaji maalumu, itaendelea hadi Septemba 8.

Raia huyo wa Iran, mwenye urefu wa mita mbili na sentimita 46, ambaye alikuwa bingwa wa Olimpiki ya Walemavu katika mpira wa wavu wa kukaa huko Rio de Janeiro na Tokyo, anatafuta medali nyingine ya dhahabu mjini Paris, lakini hawezi kulala kwenye vitanda vya Kijiji cha Olimpiki kwa sababu vitanda vyake havimtoshi.

Katika Michezo ya Olimpiki ya Walemavu nchini Japani mwaka wa 2021, taasisi husika zilibuni kitanda maalumu kwa ajili ya mwanariadha huyo wa Iran ambaye ni mtu wa pili kwa urefu zaidi duniani.

Mehrzad, Tokyo

Mkurugenzi wa timu ya taifa ya mpira wa wavu wa kukaa ya Irani, Hadi Rezaei, amesema: "Morteza Mehrzad hakupata kitanda cha kibinafsi, kama ilivyokuwa huko Tokyo, hivyo inamlazimu kulala chini. Lakini ana lengo muhimu sana akilini mwake, nalo ni kuibuka na ubingwa.”

Wakati Mehrzad alipokuwa na umri wa miaka 16, alikuwa na urefu wa mita 1.90. baadaye aligunduliwa kuwa na ugonjwa sugu wa akromegali, ambao husababisha mwili kutoa homoni nyingi za ukuaji.

Katika umri huo, alianguka chini alipokuwa akiendesha baiskeli na kupata jeraha kubwa kwenye fupanyonga (pelvis) yake.

Morteza Mehrzad, Rio de Janeiro

Mehrzad alifanyiwa upasuaji mara kadhaa, na tangu wakati huo mguu wake wa kulia uliacha kukua na kuwa mfupi zaidi kwa sentimeta 15 kuliko wa kushoto, jambo lililofanya iwe vigumu kwake kutembea bila tatizo, na akalazimika kutumia kiti cha magurudumu (wheelchair).