Sep 10, 2024 11:17 UTC
  • Iran yaihimiza zaidi jamii ya kimataifa iilazimishe Israel ikomeshe jinai zake

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameitaka jamii ya kimataifa na taasisi zenye ushawishi kimataifa hususan Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuulazimisha utawala wa Kizayuni ukomeshe jinai zake huko Ghaza na katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Mapema leo Jumanne, Nasser Kan'ani amelaani vikali jinai mpya zilizofanywa na Israel katika kambi ya wakimbizi ya Khan Yunis huko Ghaza na kuua kwa umati makumi ya Wapalestina wasio na hatia.

Amegusia pia ushahidi unaoonesha kwamba Israel inatumia mabomu na silaha zilizopigwa marufuku kuwashambulia wananchi wasio na ulinzi wa Palestina na kusema kuwa, utawala wa Kizayuni unafanya mashambulizi ya kiwendawazimu dhidi ya raia wa Palestina tena katika kambi za wakimbizi na kwa mara nyingine umeonesha jinsi usivyojali sheria yoyote ya kimataifa wala msingi wowote wa kimaadili na kibinadamu.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran vilevile amesisitiza kuwa, jinai zinazotia kichefuchefu zinazofanywa na utawala wa Kizayuni za kuangamiza kizazi cha watu wasio na hatia ni jinai za kvita na ni hatari kwa usalama wa dunia nzima.

Wakati huo huo makundi ya Muqawama ya Palestina ikiwa ni pamoja na Kamati ya Muqawama na Harakati ya Demokrasia kwa ajili ya Ukombozi wa Palestina zimesema kuwa, jinai hiyo mpya ya Israel ya kushambulia mahema ya wakimbizi wa Palestina huko Khan Yunis, kusini mwa Ukanda wa Ghaza imefanyika kwa uungaji mkono kamili wa Marekani kwa shabaha ya kuangamiza kizazi cha Palestina. 

Shambulio la kikatili la leo Jumanne lililofanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya mahema ya wakimbizi wa Palestina kusini mwa Ukanda wa Ghaza limeua shahidi Wapalesitna wasiopungua 40 na kujeruhi wengine zaidi ya 60.

Tags