Tathmini ya vipengele vya kijeshi vya Operesheni ya Ahadi ya Kweli -2: Jibu kwa shari za Israeli
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) jana usiku lilitoa taarifa likitangaza kuwa limeshambulia kitovu cha maeneo yanayokaliwa kwa mabavu ya Palestina (Israel) ikiwa ni katika kujibu mauaji ya shahidi Ismail Haniyeh, Sayyid Hassan Nasrullah na Meja Jenerali Abbas Nilforoushan Kamanda na mshauri wa ngazi ya juu wa IRGC huko Lebanon.
Oparesheni hiyo kwa jina la Ahadi ya Kweli nambari 2 imetekelezwa kwa idhini ya Baraza Kuu la Usalama wa Taifa na baada ya kujulishwa kamandi kuu ya vikosi vya ulinzi na kuungwa mkono na jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Wizara ya Ulinzi.
Jeshi la IRGC limeonya kuwa: Iwapo utawala wa Kizayuni utachukua hatua za kijeshi kujibu operesheni hiyo ambayo imetekelezwa kwa msingi wa haki za kisheria za nchi na sheria za kimataifa, utakabiliwa na mashambulizi makubwa haribifu zaidi.
Meja Jenerali Mohammad Bagheri Mkuu wa Majeshi ya Iran ameashiria kuhusu oparesheni ya makombora ya jeshi la IRGC katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na kusema: 'Jana usiku kikosi cha anga cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) kililipiza kisasi kwa jinai nyingi za Wazayuni, kupitia oparesheni yake ya kishujaa.'
Meja Jenerali Bagheri ameeleza kuwa oparesheni hiyo haikuvilenga vituo vya kiuchumi na viwanda vya utawala wa Kizayuni wala raia wa kawaida katika ardhi hizo zinazokaliwa kwa mabavu (Israel); katika hali ambayo hilo lingewezekana kikamilifu. Amesema, Jeshi la IRGC na vikosi vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran viko tayari iwe ni katika uga wa kiulinzi au kushambulia na kuwa vipo tayari kukariri mashambulizi yao tena kwa mara kadhaa. Amesema iwapo utawala wa Kizayuni ambao umefikia kiwango cha uwendawazimu hautadhibitiwa na Marekani na nchi za Ulaya na kutaka kuendeleza jinai zake au kuchukua hatua za kukiuka mamlaka ya kujitawala ya Iran, basi Iran itatekeleza tena kwa nguvu zaidi oparesheni kama ya Jumanne usiku na kushambulia miundo mbinu yote ya utawala huo. Meja Jenerali Bagheri amesema anataraji kuwa Marekani itaachana na mbinu yake ya zamani na kuushinikiza utawala wa Kizayuni ili eneo hili lipate amani.

Tofauti kuu kati ya Oparesheni ya Ahadi ya Kweli nambari 2 na oparesheni ya kabla yake ni kusambaratishwa kambi za jeshi la anga la utawala wa Kizayuni kama sehemu ya kistratejia ya jeshi la Israel na maeneo yanayolindwa vikali kuhusu taarifa za oparesheni za makombora. Afisa mmoja wa Marekani amedai kuwa Iran Jumanne usiku ilivurumisha katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu (Israel) jumla ya makombora 220 katika mawimbi mawili ya oparesheni. Taarifa nambari mbili ya IRGC imesisitiza kuwa vituo vya kimkakati ndani ya ardhi zinazokaliwa kwa mabavu (Israel) vimelengwa kwa makombora na kwamba baadhi ya kambi za jeshi la anga na vituo vya rada, vituo ambavyo Israel imekuwa ikivitumia kuratibu njama na mauaji dhidi ya viongozi wa muqawama na hasa Ismail Haniyeh na Sayyid Hassan Nasrullah na makamanda wengine wa kijeshi wa Hizbullah, muqawama wa Kiislamu wa Palestina na makamanda wa jeshi la IRGC vimepigwa na kuharibiwa kwa makombora. Pamoja na kuwa maeneo hayo yalikuwa yakilindwa kwa mifumo ya ulinzi ya kisasa na hali ya juu lakini asilimia 90 ya makombora ya Iran yamepiga na kulenga shabaha kama ilivyokusudiwa. Video zilizosambaa za makombora ya balistiki yaliyorushwa na Iran dhidi ya Israel zinaonyesha kuwa makombora mengi yalilenga shabaha zao, ambapo mfumo wa ulinzi wa "Kuba la Chuma" wa Israel haukuweza kuzuia makombora hayo.
Iran imezishambulia kambi 3 kuu za anga za jeshi la utawala wa Kizayuni ikiwemo kambi ya jeshi la anga ya Nevatim huko Negev ambazo zilikuwa zikitumika kuegeshea ndege aina ya F-35 na pia kambi ya jeshi la anga la Israel ya Hatsarim ambayo ilitumika kama kituo cha kutekeleza mauaji dhidi ya Sayyid Hassan Nasrullah. Makao makuu ya Shirika la Ujasusi la utawala wa Kizayuni (Mossad) ambayo yamekuwa yakitumiwa kama kituo cha kupanga na kuendeshea mauaji, rada za kimkakati na pia kambi nyingine za kuegesha vifaru na magari ya kijeshi karibu na Ukanda wa Gaza zimeshambuliwa.

Nukta muhimu ya kuzingatia hapa ni namna Iran ilivyotumia makombora ya kisasa ya Balistiki ya Khaybar Shekan na ya Hypersonic ya Fattah katika operesheni ya jana dhidi ya Israel. Kikosi cha anga cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) kimetumia uzoefu wa oparesheni ya Ahadi ya Kweli-1 na udhaifu wa mifumo ya ulinzi ya kuzuia makombora ya utawala wa Kizayuni katika oparesheni yake ya Ahadi ya Kweli-2 kwa kustafidi na makombora yake ya kisasa ya Balistiki khususan lile la "Khaybar Shekan" na la Hypersonic la "Fattah"; ambapo kulingana na ushahidi uliopo yamesabisha vipigo vikali kwa utawala wa Kizayuni.
Kombora la Khaybar Shekan lililozinduliwa mwaka 2022 ni kombora linaloongozwa na fueli mango na linaweza kupiga shabaha umbali wa kilomita 1,450. Miongoni mwa sifa za kipekee zinazotofautisha kombora la Khaybar Shekan na makombora mengine ya Iran ni kichwa chake ambacho huruka kwa kutumia mbawa za aerodynamic na kukwepa baadhi ya mifumo ya ulinzi wa anga.
Kombora la Hypersonic la "Fattah- 2" lina uwezo wa kuruka kwa kasi ya juu na lina mabawa ambayo yametengenezwa kwa mfumo wa Hypesonic Glide vehicle HGV. Ni nchi 4 tu duniani, ikiwa ni pamoja na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambazo zina teknolojia ya aina hii ya silaha za Hypersonic. Komborala Fattah-2 lina kasi kubwa na uwezo wa aina yake katika kubadilisha mkondo wake likiwa angani na hivyo kumhadaa adui na kuweza kukwepa mitego yake.

Kiujumla tunaweza kusema kuwa operesheni ya makombora ya Ahadi ya Kweli- 2 katika uga wa kijeshi imeweza kuthibitisha hatua kubwa iliyopiga Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika utendaji wa mifumo ya makombora yake mkabala wa madai matupu ya utawala wa Kizayuni ya eti kutopenyeka mifumo yake ya ulinzi wa makombora hasa mfumo wake wa kuzuia makombora wa Arrow ambao kwa muda mrefu umekuwa ukisifiwa kwa ufanisi wake wa kuzuia hujuma za makombora ya balestiki.