Araghchi: Iran itatoa majibu kwa Israel katika wakati itakaoona unafaa
(last modified Mon, 28 Oct 2024 02:57:46 GMT )
Oct 28, 2024 02:57 UTC
  • Araghchi: Iran itatoa majibu kwa Israel katika wakati itakaoona unafaa

Sayyid Abbas Araghchi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesisitiza kuwa, ni haki ya Jamhuri ya Kiislamu kujibu uchokozi wa utawala wa Kizayuni na itatoa majibu dhidi ya Israel katika muda itakaoona unafaa.

Hayo yamesemwa na Ebrahim Rezaei, Msemaji wa Kamati ya Usalama wa Taifa na Siasa za Nje ya Bunge la Iran wakati alipohojiwa na shirika la habari la Tasnim na kuongeza kuwa, Abbas Araghchi amesema hayo katika kikao alichofanya jana mchana na kamati hiyo.

Rezaei ameongeza kuwa, katika kikao hicho, Mheshimiwa Araghchi ametoa ripoti fupi kuhusu hali ilivyo hivi sasa katika eneo hili ikiwa ni pamoja na hali ya kambi ya muqawama na uadui wa utawala wa Kizayuni pamoja na safari zake za mfululizo alizozifanya hivi karibuni kuzitembelea nchi za ukanda huu.

Msemaji wa Kamati ya Usalama wa Taifa na Siasa za Nje ya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) amesisitiza kuwa, Bw. Araghchi amezungumzia pia moyo na mori walionao wanamapambano wa kambi ya Muqawama katika kuendeleza mapambano dhidi ya Israel na kusema kuwa, ni kweli viongozi wa ngazi za juu wa kambi hiyo wameuawa shahidi lakini Muqawama bado uko imara na unazidi kuwa imara siku baada ya siku. 

Pia amesema, lengo la utawala wa Kizayuni ni kuzusha vita vikubwa vya pande zote, Iran haitaki vita, lakini haiogopi kuingia vitani kulinda haki zake na imejiandaa kwa lolote.