Rais Pezeshkiani: Leo hii tunakabiliwa na vita kamili vya kiuchumi
(last modified Mon, 04 Nov 2024 12:43:28 GMT )
Nov 04, 2024 12:43 UTC
  • Rais Pezeshkiani: Leo hii tunakabiliwa na vita kamili vya kiuchumi

Akizungumzia kukabiliwa na vita kamili vya kiuchumi, Rais Daktari Masoud Pezeshkian wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema: 'Maadui wanajaribu kututia mtegoni kupitia matatizo ya kiuchumi, lakini kamwe hawatafanikiwa.'

Kwa mujibu wa Kanali ya Sahab, Rais Masoud Pezeshkian aliyekuwa akizungumza leo katika hafla ya kuwaenzi wahusika na wasimamizi wa Mpango wa Kunyanyua Uzalishaji nchini, ameeleza kuwa, tunachokabiliana nacho leo hii ni vita kamili vya kiuchumi na kuongeza kuwa: 'Hatuogopi vita vya kijeshi, wanajua kwamba hawawezi kutushinda katika sekta hii, nyinyi mmempiga adui kwa ngumi hii kali kwa kuzalisha ngano na mazao mengine mengi.'

Rais Pezeshkian, ameendelea kusema kuwa: "Vita vya leo ni vita vya kiuchumi, sio vita vya mabomu na makombora. Tuna makombora ya kuwafanya wasithubutu kutushambulia, hatuna makombora ya kushambulia mtu wala kuteka nchi za watu."

Masoud Pezeshkian amesema kwamba tumetengeneza makombora ambayo yatamzuia mtu yeyote kushambulia wakati wowote, na sehemu yoyote kama inavyofanya Israel huko Gaza. Ameongeza kuwa, ni heshima na utukufu kwa watu wa Gaza kwamba Israel haijaweza kuwafanya wasalimu amri, licha ya kuwa kwa muda wa mwaka mmoja sasa, imetumia kila njia na kutenda kila aina ya jinai za kinyama dhidi yao.

Rais wa Iran amesema nchini Iran muhalifu aliyeua watu 10 anapohukumiwa na kuadhibiwa kisheria, hutwambia kuwa mmekiuka haki za binadamu! Amekosoa vikali mienendo ya nchi za Magharibi dhidi ya jinai nyingi zinazofanywa na utawala wa Kizayuni za kuwaua shahidi wanawake na watoto wa Kipalestina.

Tangu kuanza kwa mashambulizi ya utawala ghasibu wa Kizayuni katika Ukanda wa Ghaza tarehe 7 Oktoba 2023, Wapalestina elfu 43, 341 wameuawa shahidi na wengine elfu 12,105 wamejeruhiwa, wengi wao wakiwa ni watoto na wanawake.