Baqaei: Vitisho, vikwazo na mashinikizo ya maadui dhidi ya Iran hayafui dafu
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran amesisitiza kuwa, vitisho, vikwazo na mashinikizo ya maadui dhidi ya Iran hayana tija.
Akizungumzia uzoefu uliofeli wa Donald Trump katika kukabiliana na Iran, msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu, Esmail Baqaei, amewashauri wapangaji wapya wa Ikulu ya White House kuwa na akili timamu na kuonya kuwa: "Ni kosa kukariri makosa."
Baqaei ameongeza kuwa: "Mazungumzo yetu si tu kwa ajili ya mazungumzo, bali yana lengo na kudhamini maslahi na usalama wa taifa wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Tunajua vyema kwamba usalama wa taifa wa Iran si tofauti na usalama wa eneo la Maghariibi mwa Asia."
Kuhusu mauaji ya kimbari yanayofanywa na Israel dhidi ya watu wa Gaza, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema, Marekani na Ujerumani ndio wadhamini wakubwa wa silaha kwa utawala wa Kizayuni wa Israel, kwa hivyo kipaumbele cha Iran ni kuisaidia jamii ya kimataifa kukabiliana na utawala huo.
Wakati huohuo, Baqaei amesema kuhusu vita vya Russia na Ukraine kwamba: "Kimsingi, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilitangaza tangu mwanzoni mwa vita hivi kwamba utumiaji mabavu haukubaliwi katika uhusiano wa kimataifa, na tunaamini kuwa nchi zinapaswa kutatua tofauti zao kwa njia za usuluhishi wa amani na za kidiplomasia; na suala la Ukraine pia linapaswa kutatuliwa kwa njia ya mazungumzo.