Rais Rouhani asisitiza mapambano dhidi ya dawa za kulevya
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza udharura wa kuzidishwa ushirikiano wa kieneo na kimataifa katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya.
Rais Rouhani ameyasema hayo leo katika mkutano wa Kamati ya Kupambana na Dawa za Kulevya hapa nchini na kusisitiza kuwa, kuna udharura wa kuimaishwa zaidi ushirikiano baina ya asasi na taasisi zote ndani ya Jamhuri ya Kiislamu kwa ajili ya kupambana na dawa za kulevya. Amesema ni muhimu sana kupanuliwa zaidi ushirikiano wa kieneo na kimataifa katika masuala ya ripoti za kipelelezi na operesheni za kupambana ipaswavyo na usafirishaji wa dawa za kulevya.
Rais Rouhani amesema masuala kama utumiaji wa uzoefu wa kimataifa, udhibiti wa kuigizwa dawa za kulevya nchini, kupambana na uzalishaji wa dawa za kulevya viwandani na kutumia zana za kisasa katika maeneo ya forodha vinapaswa kupewa kipaumbele zaidi katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya.