Mashauriano ya Iran na Ethiopia ya kupanua uhusiano wa kiuchumi
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayeshughulikia masuala ya Bunge amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri Mshauri katika Wizara ya Masuala ya Kigeni ya Ethiopia ambapo wamejadiliana njia za kupanua ushirikiano wa kiuchumi baina ya nchi hizi mbili ikiwemo uanachama katika kundi la "BRICS".
Vahid Jalalzadeh, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje anayeshughulikia Masuala ya Majlis na Wairani wanaoishi nj ya nchi katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alikutana siku ya Ijumaa na Mesganu Arga Moach, Waziri Mshauri katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Ethiopia mjini Addis Ababa ( mji mkuu wa Ethiopia) ambapo walijadili masuala tofauti yanayozihusu nchi mbili. Walibadilishana maoni kuhusu upanuzi wa ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi hizi kupitia Tume ya Pamoja ya Uchumi na Ushirikiano wa Kusini-Kusini kupitia ya wanachama wa BRICS.
Waziri huyo wa Ethiopia alisisitiza katika mkutano huo kuwa: Iran na Ethiopia zina ushirikiano mkubwa katika sekta mbalimbali zikiwemo biashara, uwekezaji, utalii na uhamishaji wa teknolojia.
Wawakilishi hao wa Iran na Ethiopia walikubaliana kuchunguza uwezekano wa kuimarisha ushirikiano wa pande mbili kupitia Tume ya Pamoja ya Uchumi.
Ikumbukwe kwamba Mohammed Baqir Qalibaf, Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran na Abi Ahmad Ali, Waziri Mkuu wa Ethiopia pia walikutana siku ya Ijumaa na kujadiliana masuala tofauti ya pande mbili. Katika mkutano huo, ulazima wa kupanua uhusiano wa pande mbili katika nyanja za kiuchumi, kiutamaduni na kisiasa na kutumia uwezo wa BRICS ulisisitizwa.