Iran yasikitishwa na shambulio la droni lililoua 70 hospitalini Darfur, Sudan
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmail Baghaei amelaani shambulio la ndege isiyo na rubani dhidi ya hospitali moja katika mji wa El Fasher katika mkoa wa magharibi wa Darfur nchini Sudan, na kusababisha vifo vya makumi ya watu.
Baghaei leo Jumatatu amelaani vikali mauaji ya raia, na wimbi la mashambulizi kwenye maeneo ya kiraia ikiwa ni pamoja na hospitali katika nchi hiyo ya Kiafrika, na kutoa wito wa kuzingatiwa kanuni na sheria za kibinadamu.
Msemaji huyo wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni wa Iran vile vile amesisitiza haja ya kusitishwa kwa mzozo unaoendelea nchini Sudan kupitia mazungumzo na suluhu ya kisiasa.
Shambulio hilo dhidi ya Hospitali ya Saudia mjini El Fasher lilifanyika siku ya Ijumaa. Shirika la Afya Duniani WHO limesema takriban watu 70 waliuawa huku na wengine 19 wakijeruhiwa katika shambulio hilo, dhidi ya kituo cha matibabu ambacho kilikuwa moja ya hospitali za mwisho kufanya kazi huko El Fasher.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus alilaani shambulio hilo, akibainisha kuwa hospitali hiyo ilikuwa na wagonjwa wengi wakati shambulio hilo lilipotokea.
Jeshi la Sudan limekuwa katika vita na kundi la wanamgambo la RSF tangu Aprili 2023. RSF inadhibiti karibu eneo lote la Darfur.