Pezeshkian: Silaha za nyuklia hazina nafasi katika doktrini ya Jamhuri ya Kiislamu
Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian amesema nchi yake haifuatilii vita wala silaha za nyuklia, kwani mafundisho ya Jamhuri ya Kiislamu yanakataa mauaji ya watu wasio na hatia kwa hali yoyote.
Rais Pezeshkian alisema hayo jana Alkhamisi na kueleza kuwa, “Vita si kwa manufaa yetu; hatutafuti silaha za nyuklia. Hii ndiyo fatwa ya Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu.” Pezeshkian amesema hayo akirejelea amri ya kidini ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, inayopiga marufuku matumizi ya nyuklia na silaha za maangamizi.
Rais ameongeza kuwa, hata wale "wanaotoa madai hayo" ndani ya Iran hawawezi kuisukuma nchi hii kuzalisha silaha za nyuklia, kwa sababu "mafundisho ya Jamhuri ya Kiislamu yanakataa mauaji ya watu wasio na hatia kwa hali yoyote ile."
Rais Pezeshkian ameyasema hayo mjini Tehran alipohutubia zaidi ya wajumbe 100 kutoka nchi za kigeni na mashirika ya kimataifa katika Maadhimisho ya mwaka wa 46 wa Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Amesema utawala wa Israel ambao umefanya vitendo vya kichokozi dhidi ya nchi zote za eneo la Asia Magharibi unaibua tuhuma zisizo na msingi dhidi ya shughuli za nyuklia za Iran.
Hii ni katika hali ambayo, "Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) umekagua vituo vya nyuklia vya Iran wakati wowote unapokusudia kufanya hivyo," Pezeshkian amesema na kuongeza kuwa, nchi yake haina tatizo na ukaguzi zaidi, kwani haina mpango wa kuzalisha silaha za nyuklia.