Mkutano wa dharura wa OIC kuhusu Gaza kufanyika kwa pendekezo la Iran
Kikao kisicho cha kawaida cha Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) ch kuchunguza njama ya Marekani na Israel ya kuwaondoa kwa nguvu watu wa Gaza, kitafanyikandani ya wiki zijazo kutokana na pendekezo la Iran.
Duru katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran zimeliambia shirika la habari la IRNA Jumatano kwamba, pendekezo la Tehran, lililowasilishwa rasmi katika barua ya Waziri wa Mambo ya Nje, Abbas Araghchi kwa Katibu Mkuu wa OIC, limekaribishwa sana na mataifa ya Kiislamu, huku kikao hicho kikitarajiwa kufanyika mapema Machi.
Iwapo utafanyika, mkutano huo utawaleta pamoja Mawaziri wa Mambo ya Nje wa OIC ambao watajadili hatua za kukabiliana na mpango wa Rais wa Marekani, Donald Trump wa kuwaondoa kwa nguvu Wapalestina kutoka Ukanda wa Gaza.
Katika siku za hivi karibuni, Araghchi ameendelea juhudi kubwa za kidiplomasia, akifanya mashauriano na viongozi wenzake kutoka Saudi Arabia, Misri, Algeria, Uturuki, Pakistan, Malaysia na Gambia, inayoshikilia uenyekiti wa sasa wa OIC.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran siku ya Jumamosi alilaani njama hiyo "hatari" ya pamoja ya Marekani na Israel na akatoa wito wa kufanyika kwa mkutano wa dharura wa OIC kushughulikia suala hilo.
"Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu lazima ichukue uamuzi madhubuti haraka iwezekanavyo kwa kufanya mkutano usio wa kawaida wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi wanachama, ili kutetea haki halali za watu wa Palestina," mwanadiplomasia huyo mkuu wa Iran alisema katika mazungumzo ya simu na Katibu Mkuu wa OIC, Hussein Ibrahim Taha.