Iravani: Iran inaunga mkono kuundwa serikali jumuishi nchini Syria
Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa amesema: Iran inaunga mkono uundwaji wa serikali shirikishi kupitia uchaguzi huru na mazungumzo jumuishi ya kitaifa nchini Syria.
Amir Saeid Iravani ameyasema hayo katika kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mjini New York kilichokadili hali ya Asia Magharibi na Syria na kuongeza kuwa: "Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa mara nyingine tena inatilia mkazo msimamo wake usioyumba wa kutetea kujitawala, uhuru, ardhi moja na kamili ya Syria."
Iravani amesema kwamba mustakabali wa Syria lazima uamuliwe na watu wa nchi hiyo wenyewe, bila ya kuingiliwa na nchi za kigeni au kulazimishwa, na ameongeza kuwa: "Utawala wa Kizayuni (Israel) unaendelea kuwa tishio kubwa kwa Syria, kwani mara kadhaa umekiuka mamlaka na ardhi ya nchi hiyo, na unaendelea kukiuka waziwazi maazimio yote ya Baraza la Usalama kwa kukataa kuondoa katika Miinuko ya Golan."
Balozi wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesema kuwa, Baraza la Usalama linapaswa kuchukua hatua madhubuti za kukomesha hujuma za utawala wa Kizayuni na kuulazimisha kuondoka katika maeneo yote yanayokaliwa kwa mabavu ya Syria.