Araqchi: Pwani ya Iran ni lango la kuunganisha uchumi wa dunia
(last modified Sun, 16 Feb 2025 13:47:32 GMT )
Feb 16, 2025 13:47 UTC
  • Araqchi: Pwani ya Iran ni lango la kuunganisha uchumi wa dunia

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa pwani ya Iran ni njia ya kuunganisha uchumi wa dunia.

Abbas Araqchi ameeleza hayo leo katika Mkutano wa 8 wa Nchi za Pambizoni mwa Bahari ya Hindi unaofanyika Muscat, mji mkuu wa Oman. Amesema kuwa, katika historia, bahari zimekuwa lango la kuunganisha ustaarabu, kuliko kuwa mipaka ya kijiografia.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameeleza kuwa Bahari ya Hindi tokea maelfu ya miaka hadi sasa imekuwa ikitumika kama njia ya majini na  njia kuu ya biashara, kubadilishana masuala ya kiutamaduni, na kuendeleza ustaarabu.

Ameongeza kuwa bahari ziliwaunganisha wafanyabiashara kutoka pwani ya India hadi Afrika, kutoka visiwa vya Indonesia hadi Ghuba ya Uajemi, na kutoka Iran hadi Bahari Nyekundu.

Mkutano wa 8 wa Nchi za Pambizoni mwa Bahari ya Hindi umeanza leo na unaendelea hadi kesho Jumatatu. Mkutano huo unaofayika chini ya kauli mbiu "Kuelekea katika Maeneo Mapya ya Ushirikiano wa Baharini" unahudhuriwa na viongozi wa ngazi ya juu kutoka nchi 20 wananachama, chini ya uenyeji wa wa pamoja wa Oman, India na Singapore. 

Mkutano huo wa Muscat, Oman unalenga kuimarisha ushirikiano kati ya nchi na taasisi mbalimbali ili kutatua changamoto za pamoja, kuimarisha mfungamano na kupanua ustawi endelevu katika kanda hiyo.