Iran yasikitishwa na shambulio la kigaidi lililoua 44 msikitini Niger
(last modified Sun, 23 Mar 2025 10:48:58 GMT )
Mar 23, 2025 10:48 UTC
  • Iran yasikitishwa na shambulio la kigaidi lililoua 44 msikitini Niger

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baghaei amelaani vikali shambulio la kigaidi la karibuni dhidi ya msikiti mmoja kusini magharibi mwa Niger.

Baghaei amesema kuwa, kitendo hicho cha kigaidi kilichotekelezwa katika sehemu takatifu na wakati wa Swala ya Ijumaa ni kinyume na misingi ya Uislamu na kinakanyaga sheria zote za kimataifa na haki za binadamu.

Msemaji huyo wa Iran amekariri msimamo wa tangu enzi wa Jamhuri ya Kiislamu wa kulaani aina zote za ugaidi na misimamo mikali ya kufurutu ada.

Amesisitiza umuhimu wa kuimarisha zaidi ushirikiano na uratibu katika ngazi mbalimbali za kikanda na kimataifa ili kuzuia na kupambana na zimwi la ugaidi.

Takriban watu 44 waliuawa huku 13 wakijeruhiwa katika shambulio hilo katika kijiji cha Fonbita katika wilaya ya kijijini ya Kokorou, lililotokea wakati wanamgambo waliotambuliwa kuwa wanachama wa Daesh katika Sahara Kubwa (ISGS) walipovamia msikiti huo, wakiwalenga waumini siku ya Ijumaa.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuna haja ya kuwafungulia mashitaka na kuwaadhibu wahusika na wachochezi wa mashambulizi ya kigaidi.

Kadhalika ametoa mkono wa pole kwa familia za wahanga wa ukatili huo, serikali na taifa la Niger kutokana na shambulio hilo la kigaidi la Ijumaa.