Iran: Vitisho vya US vinakinzana na wito wake wa diplomasia
Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian amekosoa lugha ya vitisho dhidi ya Tehran, akisisitiza kuwa nchi hii iko tayari kufanya mazungumzo lakini "katika mazingira ya usawa."
Pezeshkian alisema hayo jana Jumamosi hapa mjini Tehran katika mazungumzo yake na Waziri wa Sayansi, Utafiti na Teknolojia wa Iran pamoja na manaibu wake na kueleza kuwa, "Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inataka mazungumzo lakini katika mazingira ya usawa."
Ameeleza bayana kuwa, "Wanaitishia Iran kwa upande mmoja na wanataka kufanya mazungumzo kwa upande mwingine. Ikiwa unatafuta mazungumzo, kwa nini unatoa vitisho? Leo, Marekani sio tu inaidhalilisha Iran bali pia ulimwengu, na tabia hii inakinzana na ombi la mazungumzo."
Kauli ya Pezeshkian imekuja baada ya Rais wa Marekani, Donald Trump kuitaka Tehran kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na Washington kuhusu mpango wake wa nyuklia huku akitishia kuishambulia Jamhuri ya Kiislamu ikiwa diplomasia itafeli.
Jumapili iliyopita, Trump kwa mara nyingine tena alitishia kuishambulia Iran kwa mabomu na kuitoza ushuru maradufu, ikiwa Tehran haitafikia makubaliano na Washington juu ya mpango wake wa nyuklia. Tayari Marekani imeleta ndege zaidi za kivita katika eneo hili la Asia Magharibi.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi siku ya Jumatano alisisitiza utayarifu wa Tehran kushiriki katika mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja na Marekani kuhusu mpango wake wa amani wa nyuklia, akionya kwamba vitisho vya Marekani havitakuwa na matokeo mengine ghairi ya "kuvuruga zaidi" hali ya sasa."
"Jamhuri ya Kiislamu, kama ilivyokuwa huko nyuma, iko tayari kwa mazungumzo ya kweli katika mazingira ya usawa na kwa njia isiyo ya moja kwa moja," Araghchi aliongeza.