Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran: Mpira sasa uko upande wa Marekani
Apr 09, 2025 06:38 UTC
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameeleza katika andiko lililochapishwa na gazeti la Washington Post: "mpira sasa uko upande wa Marekani, na ikiwa Washington inatafuta suluhu ya kweli ya kidiplomasia, sisi tayari tumeshatangulia kuonyesha njia ya kuifikia."
Sayyid Abbas Araghchi, amebainisha katika makala hiyo: "katika wiki za hivi karibuni yamekuwapo mabadilishano ya barua na jumbe kati ya Iran na Marekani; na kinyume na baadhi ya tafsiri za kijuujuu zilizotolewa, mawasiliano hayo, kwa uchache kutokea upande wetu sisi, hayajawa ya kiishara tu wala ya kimaonyesho. Iran inazichukulia hizo kuwa ni jitihada halisi za kubainisha misimamo kwa uwazi kabisa na kufungua njia ya fursa kuelekea kwenye diplomasia".
Araghchi ameashiria matamshi aliyotoa Rais Donald Trump wa Marekani siku ya Jumatatu na akabainisha kwa kusema: "Iran iko tayari kwa dhati kutafuta njia ya maelewano kwa lengo la kufikia makubaliano; na tutakutana nchini Oman siku ya Jumamosi kwa mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja, ambayo mbali na kuwa ni fursa, yatakuwa ni mtihani wa kupimwa pia".
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameendelea kueleza katika andiko lake hilo: "kigezo tunachopendekeza sisi kwa ajili ya mashauriano haya sio ubunifu mpya au hakijawahi kutokea. Marekani yenyewe sasa hivi inapatanisha kwa mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Russia na Ukraine, ambao ni mzozo mkali zaidi na tata zaidi unaojumuisha nyanja za kimkakati, ardhi, kijeshi, usalama na kiuchumi".
Araghchi ameongezea kwa kusema: "kufuatilia kufanya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja si taktiki wala matokeo ya mwelekeo wa kiitikadi, bali ni chaguo la kimkakati linalofanywa kwa kuzingatia tajiriba. Sisi tunakabiliana na ukuta mkubwa wa kutokuwa na imani na tuna shaka kubwa juu ya kuwepo nia ya kweli. Ni shaka ambazo zimezidishwa na kukazania Marekani kuanzisha tena sera yake ya "mashinikizo ya juu kabisa" kabla ya kutafuta maelewano yoyote ya kidiplomasia.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran aidha amekumbusha kwamba, ili kupiga hatua kuelekea kwenye mustakabali, ni lazima kwanza tufikie kwenye uelewa wa pamoja juu ya ukweli kwamba, kimsingi, hakuna kitu kinachoitwa "chaguo la kijeshi," achilia mbali "suluhisho la kijeshi."
Kuhusiana na hilo Sayyid Abbas Araghchi amefafanua: "kutumia rasilimali za fedha za walipakodi wa Marekani kwa ajili ya kushadidisha uwepo wa kijeshi wa Marekani katika eneo letu la (Asia Magharibi), uwepo ambao unaweza kuhatarisha maisha ya wanajeshi wa Marekani kwenye eneo la maelfu ya kilomita kutoka ardhini kwao, sio tu haufikii kwenye natija ya kidiplomasia, bali ni kikwazo kwa hilo; na taifa lenye kuheshimika la Iran halitakubali kamwe kuburuzwa na kulazimishwa.../
Tags