Pezeshkian: Iran, Saudia zinaweza kuwa kielelezo cha ushirikiano wa kikanda
(last modified Fri, 18 Apr 2025 07:16:26 GMT )
Apr 18, 2025 07:16 UTC
  • Pezeshkian: Iran, Saudia zinaweza kuwa kielelezo cha ushirikiano wa kikanda

Rais wa Iran Masoud Pezeshkian wa Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu na Saudi Arabia zinaweza kuwa kielelezo cha ushirikiano wa kieneo na kusisitiza kuwa, umoja wa nchi za Kiislamu ni sharti la kupatikana amani, usalama na maendeleo endelevu ya kiuchumi katika eneo hili.

Pezeshkian aliyasema hayo jana Alkhamisi jioni alipokutana na Waziri wa Ulinzi wa Saudia, Mwanamfalme Khalid bin Salman na ujumbe wake mjini Tehran, saa chache baada ya Waziri huyo wa Saudia kuwasili katika mji mkuu wa Iran ili kujadili maendeleo ya kieneo na uhusiano wa pande mbili na viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu.

Rais wa Iran ametilia mkazo uhusiano wa kina wa kidini, kiutamaduni na kihistoria kati ya nchi za Kiislamu na kusisitiza ulazima wa kuimarishwa umoja na mafungamano katika ulimwengu wa Kiislamu.

"Tunakuangalieni kama ndugu zetu, na tangu mwanzo wa uongozi wa serikali hii, tumefanya juhudi za kuimarisha uhusiano wa kidugu kati ya mataifa ya Kiislamu," Pezeshkian amesema na kuongeza kwamba, ikiwa nchi za Kiislamu zitafikia kauli moja na umoja wa kweli, utawala wa Kizayuni hautawezi tena kusababisha maafa ya kibinadamu kama yale yanayotokea katika Ukanda wa Gaza. Pia amesisitizia umuhimu wa kuweka kando tofauti na kuimarisha ushirikiano wa kikanda.

"Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imejiandaa kikamilifu kupanua uhusiano wake na Saudi Arabia katika nyanja zote na kupanua ushirikiano wa pande mbili na nchi nyingine za Kiislamu," Pezeshkian amesisitiza.

Vile vile amepongeza wazo la kuanzisha vikundi vya kazi vya pamoja katika maeneo mbalimbali ya kisiasa, kiuchumi na kiusalama kati ya Iran na Saudi Arabia.

Mwanamfalme Khalid bin Salman kwa upande wake, ameonyesha furaha yake ya kuzuru Iran na akawasilisha salamu za dhati za baba yake, Mlinzi wa Misikiti Miwili Mitakatifu, na kaka yake, Mrithi wa Ufalme, kwa Rais wa Iran.

"Mikutano yetu na maafisa wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ya manufaa sana, chanya, na yenye kujenga," Waziri wa Ulinzi wa Saudia amebainisha.