"Msimamo wa ujasiri wa Papa Francis dhidi ya dhulma hautasahaulika"
(last modified Thu, 24 Apr 2025 10:38:57 GMT )
Apr 24, 2025 10:38 UTC

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Masuala ya Kisiasa wa Iran amesema, mchango wa Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani aliyeaga dunia hivi karibuni, Papa Francis ambaye daima alikuwa mstari wa mbele kusaidia wanyonge na wahanga wa unyanyasaji na ukatili, na vile vile misimamo yake ya kijasiri dhidi ya ukandamizaji, dhulma, ubaguzi na unyanyasaji kamwe haitasahaulika.

Wakati akitia saini kitabu cha salamu za rambirambi katika ubalozi wa Vatican hapa mjini Tehran kwa mnasaba wa kuaga dunia Papa Francis, Majid Takhte Ravanchi kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi na serikali, ametoa salamu za pole kwa balozi na viongozi wa Vatican, na Wakristo wote duniani na wafuasi wa kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki, na kumuombea amani kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Katika mazungumzo na Balozi wa Vatican hapa Tehran, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran katika Masuala ya Kisiasa mbali na kumuenzi, lakini pia amepongeza na kusifu shakhsia ya Papa Francis, akisisitiza atakumbukwa kwa misimamo yake katika kukuza na kuimarisha amani na umoja kati ya mataifa mbali mbali, na pia kushajiisha mazungumzo na maelewano kati ya wafuasi wa dini za Mbinguni duniani.

Takhte Ravanchi ambaye amewahi kuwa Balozi wa Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesisitiza kuwa, Papa Francis, ni shakhsia wa kupigiwa mfano ambaye dunia haitasahau mchango wake.

Papa alipokutana na Ayatullah Sistani

Naibu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran ameongeza kuwa, Papa daima alijitolea kuwasaidia wanyonge na wahanga wa unyanyasaji na ukatili, na misimamo yake ya kijasiri dhidi ya dhuluma, ubaguzi na dhuluma katu haitasahaulika.

Mazishi na maziko ya Papa Francis aliyefariki dunia Jumatatu iliyopita, yanatazamiwa kufanyika siku ya Jumamosi. Viongozi wa ngazi za juu kutoka nchi mbalimbali za ulimwengu wanatarajiwa kushiriki maziko hayo.