Iran yaonya; Israel inataka 'kuvuruga diplomasia' kupitia hujuma, mauaji ya kigaidi
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Sayyid Abbas Araghchi ameonya kwamba, utawala wa Kizayuni wa Israel na makundi fulani yenye maslahi maalumu huenda yakajaribu "kuvuruga diplomasia" kupitia vitendo vya hujuma na mauaji ya kigaidi wakati huu ambapo Jamhuri ya Kiislamu na Marekani zinafanya mazungumzo ya kufikia makubaliano kuhusu shughuli za nyuklia za taifa hili.
Araghchi amesema vyombo vya usalama vya nchi hii viko macho na vimewekwa katika hali ya tahadhari kutokana na uzoefu wake wa majaribio ya hujuma na mauaji ya kigaidi yaliyofanywa huko nyuma na Wazayuni.
"Majaribio ya utawala wa Israel na makundi fulani ya Maslahi Maalum ya kuharibu diplomasia - kwa kutumia mbinu mbalimbali - yapo wazi kwa watu wote kuona," Araghchi amesema hayo katika ujumbe alioutuma kwenye mtandao wa kijamii wa X siku ya Jumatano.
Amebainisha kuwa, vyombo vya usalama vya Iran viko katika hali ya tahadhari kwa kuzingatia matukio ya huko nyuma ya majaribio ya hujuma na mauaji ya kigaidi na kusisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu itatoa 'jibu halali' iwapo kutatokea kitendo chochote cha uchokozi.
Hali kadhalika, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ametahadharisha pia kuhusu propaganda chafu na kampeni ya upotoshaji iliyoelekezwa dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.
"Wale wanaotaka kupotosha fikra na maoni ya umma wanaweza pia kutarajiwa kubuni madai ya kustaajabisha na kubuni vitu kama vile picha za satelaiti zenye sura ya kuogofya," Araghchi amesema.
Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Iran amesisitiza kuwa, shughuli za amani za nyuklia za nchi hii na uwezo wake wa kurutubisha madini ya urani ziko chini ya uangalizi wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA).
Araghchi ameongeza kwa kusema, "Hali halisi: Kila miligramu moja ya urani iliyorutubishwa nchini Iran iko chini ya usimamizi na ufuatiliaji wa mara kwa mara wa IAEA."