Afrika; Mshirika wa mkakati wa thamani kwa Iran
Katika Mkutano wa Tatu wa Ushirikiano wa Kiuchumi kati ya Iran na Afrika, ulioanza katika Ukumbi wa Mikutano ya Wakuu wa Nchi za Kiislamu kwa ushiriki wa wawakilishi kutoka nchi 38 na wajumbe 51 rasmi, Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, alisisitiza kuwa Iran iko tayari kushirikiana na nchi za Afrika kwa kuwezesha nchi za Afrika zinufaika mafanikio ya Iran katika sekta za afya, biashara, viwanda, kilimo, usalama, amani na utulivu.
Kuimarisha uhusiano na nchi za Afrika ni miongoni mwa nguzo muhimu na za kudumu katika sera ya mambo ya nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Mwelekeo huu unatokana na sababu mbalimbali.
Kwa mtazamo wa kisiasa, nchi nyingi za Afrika zimepitia historia ya unyonyaji wa kikoloni, hali ambayo imewajengea ari na malengo ya kupinga ukoloni. Katika muktadha huu, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa mfano wa kuigwa kwa mataifa haya.
Aidha nchi nyingi za Afrika zina idadi kubwa ya Waislamu, na hivyo zinakaribisha kwa furaha upanuzi wa mahusiano ya kiutamaduni na kidini na Iran.
Zaidi ya hayo, bara la Afrika linajulikana kama "Bara la Fursa" kwa mtazamo wa kiuchumi. Iran, ambayo imeweka kipaumbele kwa kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na nchi rafiki hasa zile za Kiislamu, inaweza kuwa mshirika wa kuaminika kwa mataifa ya Afrika.
Katika muktadha huu, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Iran, Mohammad Reza Aref, akizungumza katika mkutano huo uliyoanza jana Jumapili mjini Tehran, alieleza kuwa: “Nawahakikishia kuwa dhamira ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kuendeleza mahusiano ya kina ya kiuchumi na Afrika.”
Aref aliongeza kuwa Afrika, kama moja ya nguzo mpya za uchumi duniani, ina thamani ya biashara ya zaidi ya dola trilioni 1.5 kila mwaka, huku ikiwa na kiwango cha ukuaji wa wastani wa asilimia 4, kinachotarajiwa kufikia asilimia 4.5 mwaka huu, na ikiwa na rasilimali asilia nyingi na idadi kubwa ya vijana, ni mshirika wa mkakati wa thamani kubwa kwa Iran.

Mkutano huu unafanyika Tehran kuanzia tarehe 26 hadi 28 Aprili na baadaye Isfahan tarehe 29 na 30 Aprili.
Uandaji wa Mkutano wa Tatu wa Ushirikiano wa Kiuchumi kati ya Iran na Afrika unaonesha dhamira thabiti ya Iran katika kukuza mahusiano yake na nchi za Afrika.
Kwa kuzingatia historia uporoaji uliofanywa na wakoloni n, nchi nyingi za Afrika kwa sasa hazijaweza kufikia ustawi unaohitajika na hivyo zinahitaji kuagiza bidhaa, huduma na wataalam kutoka nje ya bara hlo. Inaonekana kuwa Iran inaweza kuwa mshirika muhimu katika juhudi hizi za maendeleo ya nchi za Afrika ili hatimaye ziweze kujitegemea kikamilifu.
Katika mkutano huu, zaidi ya wafanyabiashara 700 kutoka nchi 38 za Afrika walisajiliwa kushiriki, huku zaidi ya maafisa 50 wa ngazi ya mawaziri na viongozi wa vyumba vya biashara kutoka Afrika wakihudhuria nchini Iran. Hii inaonesha wazi hamu na nia ya mataifa ya Afrika kuimarisha mahusiano yao na Iran.
Kwa kumalizia, inafaa kukumbusha kuwa washindani wa Iran katika bara la Afrika – yaani Saudi Arabia, Uturuki, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na Qatar – pia wamewekeza kwa kiwango kikubwa katika bara hili.
Utekelezaji wa makubaliano na mikataba iliyotiwa saini ni muhimu katika kuinua nafasi ya Iran katika nchi za Afrika.