Qalibaf: Uhai wa utawala wa Kizayuni unategemea mauaji na jinai
(last modified Tue, 29 Apr 2025 12:22:26 GMT )
Apr 29, 2025 12:22 UTC
  • Qalibaf: Uhai wa utawala wa Kizayuni unategemea mauaji na jinai

Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (Bunge) ameyataja matamshi ya utawala wa Kizayuni wa Israel kuwa ni hila isiyo na thamani inayolenga kuvuruga mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Iran na Marekani na kusema: "Hata asilimia ndogo ya uchokozi dhidi ya Iran itatambuliwa kuwa ni sawa na kuwasha moto pipa la baruti ambalo litalipua katika eneo hili."

Muhammad Qalibaf amesema leo kabla ya kikao cha Bunge kwamba Waziri Mkuu mtenda jinai wa utawala wa Kizayuni wa Israel kwa mara nyingine tena amechagua njia ya kubwabwaja na kulitishia taifa kubwa la Iran ili kuzuia anguko lake la kisiasa.

Qalibaf ameeleza haya siku mbili baada ya Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, kutaka kuharibiwa kikamilifu miundombinu ya nyuklia ya Iran. 

Qalibaf ameongeza kuwa: Utawala wa Kizayuni unategemea mauaji na jinai ili ubakie hai na unapata wazimu na kuchanganyikiwa kwa kuwepo amani na utulivu. 

Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran ameongeza kusema: Sura halisi ya utawala kandamizi wa Kizayuni imefichuliwa kwa walimwengu, hasa kwa vijana wa Marekani na Ulaya, baada ya miongo kadhaa ya upotoshaji na propaganda za  vyombo vya habari. "Utawala huu hauna fahari yoyote zaidi ya kulipua shule na hospitali kwa mabomu, na haujafikia malengo yoyote iliyoyatangaza mwanzoni mwa vita na mauaji yake ya kimbari dhidi ya Wpaalestina," amesema Qalibaf.

Qalibaf amesema: Mhalifu huyu fisadi amethibitisha katika maisha yake yote ya kisiasa kwamba mara zote anapojisifu zaidi, hukabiliwa na kushindwa pakubwa . 

 "Jinamizi la Hamas limemchanganya zaidi kuliko hapo awali, na anadai kuwa amemeza mfupa ambao kwa hakika ni mkubwa kuliko koo lake", amesema Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran.