Seddiqi: Teknolojia ya nyuklia ni mtaji wa taifa/kuna udharura wa kuwaheshimu walimu na wafanyakazi
(last modified Fri, 02 May 2025 11:14:24 GMT )
May 02, 2025 11:14 UTC
  • Seddiqi: Teknolojia ya nyuklia ni mtaji wa taifa/kuna udharura wa kuwaheshimu walimu na wafanyakazi

Khatibu wa Sala ya Ijumaa ya leo ya hapa mjini Tehran ameashria mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja ya nyuklia kati ya Iran na Marekani yaliyoanza wiki kadhaa zilizopita na kusema: Timu ya mazungumzo ya Iran ina uzoefu mkubwa; na katika mazungumzo hayo inatetea kwa nguvu na irada kamili haki ya Iran ya kumiliki teknolojia ya amani ya nyuklia ambayo ni mtaji wa taifa.

Hujjatul Islam Walmuslimin Kadhim Seddiqi amesema hayo leo katika khutba za Sala ya Ijumaa ya wiki hii hapa Tehran iliyosaliwa katika eneo la Chuo Kikuu cha Tehran na kuongeza kwamba: Timu ya mazungumzo ya Iran iliyopata ibra ya mazungumzo ya JCPOA, hivi sasa inafanya mazungumzo chini ya usaidizi na uongozi wa viongozi wa ngazi ya juu wa serikali. Teknolojia ya nyuklia ni muhimu kwetu na ni mtaji wa taifa ambao kamwe hauwezi kufumbiwa macho. 

Akiendelea na hotuba yake, Khatibu wa Sala ya Ijumaa hapa Tehran ameashiria umuhimu na nafasi maalumu ya walimu katika kuelimisha viongozi wa baadaye wa nchi; na akaitaja Wizara ya Elimu kuwa taasisi muhimu ya serikali na kituo muhimu kwa mfumo na nchi kwa ujumla. Hujjatul Islam Walmuslimin Seddiqi amesisitizia pia udharura wa serikali kuwadhaminia mahitaji yao walimu humu nchini. 

Hujjatul Islam Walmuslimin Seddiqi amesisitiza pia kuwa ipo haja ya kufuatilia utekelezaji wa waraka wa mabadiliko ya elimu kupitia Waziri na Wakurugenzi wa wizara hiyo na kuongeza kuwa: Walimu wana haki juu yetu sote, na wamekuwa na mchango katika wasomi, maafisa na viongozi wa nchi, kwa hivyo kuna  umuhimu kwa serikali kutoa kipaumbele na kuzingatia vilivyo hali ya maisha ya wapendwa wetu hawa.