Jenerali: Maadui watalipa gharama isiyoweza kuelezeka wakihujumu Iran
Mkuu wa Majeshi ya Iran, Meja Jenerali Mohammad Hossein Bagheri, ameonya kuwa hatua yoyote ya uadui dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu, ikiwemo ukiukaji wa anga ya taifa, itawaletea maadui gharama kubwa isiyoweza kufidiwa.
Meja Bagheri alitoa kauli hiyo baada ya mkutano wa ngazi ya juu wa vitengo vya ulinzi wa anga jijini Tehran mnamo Jumatatu.
Ameendelea kusema: "Wale wenye nia mbaya dhidi ya taifa la Iran na maadui wanapaswa kufahamu kuwa ukiukaji wowote wa anga yetu utawaletea madhara makubwa, na utawasababishia hasara zaidi ya matarajio yao."
Meja Bagheri alisisitiza maendeleo makubwa yaliyopatikana katika kuimarisha uwezo wa ulinzi wa anga ndani ya mwaka uliopita.
Aliweka wazi kuwa baadhi ya vitengo vya ulinzi wa anga vimeimarika mara tano ikilinganishwa na mwaka uliopita, hususan katika idadi ya radar, mifumo ya ufuatiliaji, na vifaa vya kugundua harakati za maadui.
Aidha, amesisitiza kuwa anga ya Iran inafuatiliwa kwa saa 24, na majeshi ya Iran yako tayari kwa asilimia 100 kukabiliana na shambulio lolote.
Jeneral Bagheri amedokeza kuwa vitengo vya ulinzi wa anga vya Iran vinadhibiti anga ya taifa kwa saa zote, huku vikijiandaa kwa hali yoyote kupitia mazoezi na mafunzo ya mara kwa mara.
Aidha amebainisha kuwa kiwango cha uwekezaji katika kuimarisha ulinzi wa anga kimeongezeka mara kadhaa.
Maafisa wa Iran wamesisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu haitasita kuimarisha uwezo wake wa kijeshi, ikiwemo nguvu zake za makombora, ambazo zinakusudiwa kwa ajili ya ulinzi pekee.