Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Kufuatia Mashambulizi ya Leo ya Utawala wa Kizayuni
Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetoa taarifa rasmi kulaani vikali uvamizi wa kijeshi uliofanywa na utawala dhalimu wa Kizayuni dhidi ya ardhi ya Iran.
Kwa mujibu wa shirika la habari la taifa (IRIB), taarifa hiyo inasema:
Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu
Enyi watu wa Iran mlioko kila kona ya taifa hili,
Taifa letu pendwa, Iran, leo mapema alfajiri limekumbwa na mashambulizi ya kijeshi yasiyo ya haki kutoka kwa utawala dhalimu na mhalifu wa Kizayuni. Kwa kukiuka mamlaka kamili ya taifa na uhuru wa kitaifa wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, utawala huo umelenga maeneo kadhaa, yakiwemo ya makazi katika mji mkuu Tehran na miji mingine, na kusababisha vifo na majeruhi miongoni mwa raia wasio na hatia, wakiwemo wanawake, watoto, na baadhi ya wahudumu waaminifu katika nyanja za ulinzi, taaluma, na teknolojia.
Wizara ya Mambo ya Nje inaungana na taifa zima kuomboleza mashujaa waliopoteza maisha yao wakilitumikia taifa hili kwa moyo wa uzalendo. Taarifa hii ni salamu za rambirambi na heshima kwa familia za mashahidi na kwa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu.
Mashambulizi haya ni ukiukaji wa wazi wa Kifungu cha 2, Ibara ya 4 ya Hati ya Umoja wa Mataifa, na hivyo ni tendo la uchokozi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Kwa mujibu wa Kifungu cha 51 cha hati hiyo, Iran inayo haki kamili ya kujilinda kwa njia yoyote itakayojiona inafaa. Vikosi vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kwa uwezo wao wote, na kwa mbinu ambazo jeshi litachagua lenyewe, halitasita kuchukua hatua za haraka na za dhahiri katika kulinda hadhi, mamlaka na uhuru wa taifa la Iran.”
"Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kama mwanachama mwanzilishi wa Umoja wa Mataifa, taasisi ambayo lengo lake kuu ni kuzuia uvamizi, ukiukaji wa amani, na vitisho dhidi ya usalama wa kimataifa, inasisitiza wajibu wa Baraza la Usalama kuchukua hatua ya haraka dhidi ya ukiukaji wa wazi wa amani na usalama wa dunia uliosababishwa na uvamizi wa utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran.
Iran inatoa wito kwa Mwenyekiti na wajumbe wa Baraza hilo kuchukua hatua za dharura katika suala hili bila kuchelewa."
Wizara pia inawakumbusha wajibu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa mujibu wa hati hiyo na inamtaka kuchukua hatua madhubuti mara moja.
Tunaziomba nchi zote wanachama wa Umoja wa Mataifa, hususan hasa mataifa jirani, nchi za Kiislamu, na wanachama wa Harakati ya Kutofungamana na Upande Wowote (NAM), kulaani vikali mashambulizi haya na kuchukua hatua za haraka, za pamoja, dhidi ya uchokozi huu hatari unaotishia amani ya dunia.
Madhara na athari zote za kisiasa, kijeshi na kiusalama kutokana na jinai hii ya utawala wa Kizayuni zitakuwa juu ya mabega ya utawala huo na wale wanaouunga mkono.
Aidha, haiwezekani kwamba mashambulizi haya ya kijeshi yamefanywa bila idhini au ushirikiano wa Marekani. Hivyo basi, serikali ya Marekani kama mfadhili mkuu wa utawala wa Kizayuni, itabeba dhima ya moja kwa moja kwa matokeo yote ya kisiasa, kijeshi, na kiusalama ya vitendo hivi vya kichokozi.