Araqchi: Marekani inahusika katika uchokozi wa utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran
(last modified Sun, 15 Jun 2025 11:52:21 GMT )
Jun 15, 2025 11:52 UTC
  • Araqchi: Marekani inahusika katika uchokozi wa utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amesema kwamba uchokozi wa utawala wa Israel dhidi ya ardhi ya Iran haungewezekana bila msaada wa Marekani, na kwamba jumbe za Rais wa Marekani katika mitandao ya kijamii ni dalili ya ushiriki huu.

Sayyid Abbas Araqchi amesema hayo wakati wa mkutano wake na mabalozi wa kigeni wanaoishi Tehran, na kusisitiza kwamba, "Tuna ushahidi mkubwa unaoonyesha jinsi majeshi ya Marekani yalivyoisaidia Israel."

Ameongeza kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel umevuka mstari mpya mwekundu, ambao ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa, na hilo limetokana na kutojali Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Mwanadiplomasia huyo mwandamizi amesisitiza kuwa: "Mashambulizi ya Israel yametokea tukiwa katika mazungumzo na Marekani, huku duru ya sita ya mazungumzo hayo ilipangwa kufanyika leo mjini Muscat. Utawala wa Kizayuni hautafuti makubaliano wala diplomasia, na uchokozi wake dhidi ya Iran katikati ya mazungumzo hayo ni uthibitisho wa hilo."

Araghchi aliendelea kubainisha kuwa, "Majibu yetu yanatokana na kanuni ya kujilinda katika mahusiano ya kimataifa, ambayo ni haki halali ya nchi yoyote. Tunatarajia Marekani italaani mashambulizi dhidi ya vituo vya nyuklia vya Iran kama ishara ya nia yake njema na kujiweka mbali na mzozo huu."

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameongeza kuwa: Hatutaki vita hivi vienee katika nchi nyingine au kwenye ukanda huu kwa njia yoyote, isipokuwa tutakapolazimishwa kujibu uchokozi.