Iran: Imani yetu kwa Marekani imeporomoka mno
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i128246
Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imesema Marekani imedhoofisha diplomasia na kukiuka sheria za kimataifa kwa mashambulizi yake ya kichokozi dhidi ya taifa hili, wakati mazungumzo ya nyuklia yalipokuwa yakiendelea, na hivyo kupunguza imani ya Iran kwa Marekani chini ya sifuri.
(last modified 2025-07-21T07:45:22+00:00 )
Jul 12, 2025 16:00 UTC
  • Iran: Imani yetu kwa Marekani imeporomoka mno

Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imesema Marekani imedhoofisha diplomasia na kukiuka sheria za kimataifa kwa mashambulizi yake ya kichokozi dhidi ya taifa hili, wakati mazungumzo ya nyuklia yalipokuwa yakiendelea, na hivyo kupunguza imani ya Iran kwa Marekani chini ya sifuri.

Esmail Baghaei, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amelaani shambulio la hivi karibuni la Marekani kama "kitendo cha fedheha na kinyume cha sheria" kilichotokea katikati ya mazungumzo ya kidiplomasia, akisema kwamba adui "ameshindwa kusimama dhidi ya mantiki ya mazungumzo na maingiliano."

Baghaei ameeleza bayana kuwa, "Sasa ni dhahiri kwa wote kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni mtetezi wa mazungumzo na diplomasia."

Amesisitiza kuwa, hakuna uhalali wa kisheria, kimaadili, au kisiasa kwa shambulio hilo, huku akitaja shambulio hilo "mfano wa wazi wa uchokozi" chini ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa.

Esmail Baghaei amebainisha kuwa, mashambulizi hayo ni ushahidi kwamba Washington haiwezi kutegemewa katika michakato ya kidiplomasia.

Mnamo tarehe 13 Juni, katikati ya mazungumzo ya nyuklia, Israel ilianzisha mashambulizi ya anga yaliyolenga maeneo ya Iran, yakifuatiwa muda mfupi na mashambulizi ya Marekani, licha ya Iran kuendelea kuonyesha nia njema na uwazi kwenye meza ya kidiplomasia.

Wakati wa hujuma hizo za kichokozi, hakukuwa na taarifa za kijasusi za kuaminika zilizoonyesha kuwa Iran ilikuwa ikitaka kuzalisha silaha za nyuklia.