Iran yalaani shambulio la kigaidi katika hospitali ya Quetta, Pakistan
Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran amelaani shambulio la kigaidi lililofanywa katika hospitali ya mji wa Quetta nchini Pakistan.
Ali Shamkhani, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran amemtumia ujumbe mwenzake wa Pakistan Nasser Khan Janjua, ambapo mbali na kulaani hujuma ya kigaidi iliyofanywa katika mji wa Quetta ametoa mkono wa pole kwa serikali na wananchi wa Pakistan kutokana na kuuawa raia kadhaa wa nchi hiyo katika tukio hilo la kigaidi na kuzifariji pia familia za watu hao waliouawa.
Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran ameashiria pia ulazima wa kupambana kwa hali zote na mizizi na chimbuko la kujitokeza na kuenea fikra za kigaidi na itikadi zinazosababisha kudhuriwa roho za watu wasio na hatia na vilevile kutiwa doa utambulisho wa Kiislamu na akasisitiza kuwa hakuwezi kuwepo na matumaini ya kuutokomeza ugaidi bila ya kuwepo jitihada za kweli za Jamii ya Kimataifa za kufunga njia ambazo makundi ya kigaidi yanazitumia kupatia fedha, silaha na wanachama na wafuasi wa kujiunga na makundi hayo.
Watu wasiopungua mia moja wameuawa na makumi ya wengine wamejeruhiwa katika miripuko ya mabomu iliyotokea leo asubuhi katika wadi ya huduma za dharura ya hospitali moja ya mji wa Quetta ulioko kusini magharibi mwa Pakistan.
Idadi kubwa ya mawakili na waandishi wawili wa habari ni miongoni mwa waliouawa huku hali za majeruhi wengi zikiripotiwa kuwa mbaya.../