Mkuu wa zamani IRGC azitahadharisha Saudia, Uturuki na Iraq, asema; mabomu ya Israel yanawasubiri
Kamanda Mkuu wa zamani wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) amezitahadharisha nchi za eneo zikiwemo Saudi Arabia, Uturuki na Iraq kwamba ziko katika hatari ya kukabiliwa na uvamizi wa Israel iwapo nchi za kanda hii zitashindwa kuunda "muungano wa kijeshi" dhidi ya utawala wa Kizayuni.
Kamanda wa zamani wa jeshi la IRGC amezitahadharisha nchi za eneo la Mashariki ya Kati zikiwemo Saudi Arabia, Uturuki na Iraq kuhusu kushambuliwa na utawala wa Kizayuni kupitia ujumbe aliotuma katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X.
Katika ujumbe wake huo, Mohsen Rezaei ameshauri kuwa Mkutano wa Dharura wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) uliopangwa kufanyika Doha mji mkuu wa Qatar leo Jumapili unaopasa kuzingatia kwa uzito uwezekano wa kutekelezwa hujuma ya uvamizi kama hiyo.
"Iwapo mkutano wa leo wa OIC huko Doha utashindwa kuchukua hatua za kivitendo kujibu hujuma za utawala wa Kizayuni dhidi ya nchi tano za Kiislamu na mauaji ya kimbari unaoyofanya huko Gaza, basi Saudi Arabia, Uturuki na Iraq pia zitarajie kushambuliwa na ndege za kivita na mabomu ya utawala huo," ameandika katika mtandao wa X Mkuu wa zamani wa IRGC.
Amesema muungano wa kijeshi unapasa kuundwa ili kukabiliana na utawala wa Kizayuni.
Kamanda wa zamani wa jeshi la IRGC ameeleza haya baada ya gazeti la Israel la Ha'aretz kutahadharisha katika ukurasa wake wa maoni kwamba kufuatia mashambulizi ya hivi majuzi ya anga dhidi ya Qatar, ambayo yalilenga viongozi wa harakati ya muqawama wa Palestina (Hamas) katika nchi hiyo ya Ghuba ya Uajemi, kulikuwa na uwezekano kwamba utawala huo ungeanzisha mkondo mpya dhidi ya Uturuki.