Iran: Kura ya 'snapback' ni batili, haina mashiko ya kisheria
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Sayyid Abbas Araghchi amesisitiza kuwa, juhudi za mataifa matatu ya Ulaya ya Uingereza, Ufaransa, na Ujerumani za kuhuisha vikwazo vya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu kwa kutumia utaratibu unaojulikana kama snapback' ni "batili na hazina mashiko yoyote ya kisheria."
Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Iran aliyasema hayo jana Ijumaa, akilihutubia Baraza la Usalama baada ya kupiga kura ya iwapo utaratibu huo unaoitwa "snapback" ndani ya makubaliano ya nyuklia ya 2015 yakiamilishwa yatarejesha vikwazo hivyo au la.
Araghchi ameyaeleza mashinikizo na msukumo huo wa kurejesha vikwazo vya Baraza la Usalama dhidi ya Iran kama "matumizi mabaya ya mamlaka."
Haya yanajiri huku Marekani na washirika wake, ikiwemo Troika ya Ulaya kupigia kura ya turufu rasimu ya azimio lililolenga kuakhirisha uamlishaji wa "snapback" wa kurejesha vikwazo vya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran ambavyo viliondolewa mwaka 2015, kwa mujibu wa makubaliano ya nyuklia kati ya Jamhuri ya Kiislamu na nchi za dunia.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameeleza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu imekuwa ikitekeleza kwa ukamilifu makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, Mkataba wa Kuzuia Uzalishaji na Uenezaji wa Silaha za Nyuklia NPT kama ilivyothibitishwa na ripoti 15 za Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA.
Hii ni katika hali ambayo, Rais Masoud Pezeshkian wa Iran akisisitiza kuwa, Tehran iko tayari kikamilifu kwa hali yoyote endapo nchi za Ulaya zitarejesha vikwazo vya Umoja wa Mataifa kupitia utaratibu wa snapback, na ameonya kwamba mazungumzo ya kidiplomasia yatakuwa hayana maana chini ya vikwazo vilivyorejeshwa.
Rais Pezeshkian ameashiria sera za upande mmoja za Marekani, akibainisha kuwa mbinu kama hizo hazilengi tu Iran bali pia nchi zote zinazokataa kufuata ajenda za Marekani.