Zarif: Ulimwengu wa Kiarabu unakabiliwa na changamoto chungu nzima
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i13174-zarif_ulimwengu_wa_kiarabu_unakabiliwa_na_changamoto_chungu_nzima
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amesema ulimwengu wa Kiarabu haswa katika eneo la Mashariki ya Kati unakabiliwa na changamoto nyingi na kwamba Jamhuri ya Kiislamu sio miongoni mwa matatizo ya nchi za Kiarabu.
(last modified 2026-02-05T09:20:29+00:00 )
Aug 13, 2016 03:38 UTC
  • Muhammad Javad Zarif, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran
    Muhammad Javad Zarif, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amesema ulimwengu wa Kiarabu haswa katika eneo la Mashariki ya Kati unakabiliwa na changamoto nyingi na kwamba Jamhuri ya Kiislamu sio miongoni mwa matatizo ya nchi za Kiarabu.

Akizungumza hapa mjini Tehran hii leo katika hafla ya kiutamaduni, Muhammad Javad Zarif, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kushindwa nchi za Kiarabu kutekeleza matakwa ya wananchi wao, kumezusha taharuki na wasi wasi mkubwa katika uliwengu wa Kiarabu na haswa nchini Saudi Arabia.

Zarif amesisitiza kuwa, kushindwa kuyakidhi mahitaji na kufikia matarajio ya wananchi wao, kumewapelekea viongozi wa nchi za Kiarabu kutumia mbinu ya kupanda mbegu za uhasama na chuki za kikabila, kikaumu na kimadhehebu miongoni mwa wananchi.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Muhammad Javad Zarif

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameongeza kuwa, mbali na mbinu hiyo ya kuzusha mipasuko ya kimadhehebu na kikaumu, viongozi wa nchi za Kiarabu wanaendeleza mbinu yao ya huko nyuma ya kutaka kuisawiri Iran kuwa chimbuko la matatizo mengi katika ulimwengu wa Kiarabu.

Muhamad Javad Zarif kadhalika ameashiria juu ya vitendo na matamshi makali ya watawala wa Aal-Saud na kubainisha kuwa, tabia hiyo inadhihirisha udhaifu wa hali ya juu wa viongozi wa Riyadh na kusisitiza kuwa, hatua zozote za kiuadui dhidi ya Tehran zitagonga mwamba.