Larijani: Trump ndiye 'muuaji mkubwa zaidi' wa Wairani
Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran (SNSC) amelaani vitisho vya Rais wa Marekani Donald Trump dhidi ya taifa hili, akimtaja mwanasiasa huyo kama mmoja wa wauaji wakubwa zaidi wa Wairani.
Ali Larijani amesema hayo akijibu ujumbe wa Trump wa Jumanne kwenye mitandao ya kijamii, akiwataka waandamanaji "watwae taasisi" (za serikali) na kwamba "msaada unakuja."
Trump pia aliwataka waandamanaji "wanakili majina ya wauaji na wanyanyasaji" na kutishia kwamba "watalipa gharama kubwa".
Kwa mara nyingine tena, Trump ametangaza wazi wazi kuunga mkono ghasia zinazoshuhudiwa nchini, na kutishia kufanya mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Iran ikiwa eti "waandamanaji wa amani" watapigwa risasi na kuuawa.
Akijibu bwabwaja na vitisho hivyo vya Trump, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran amesema kuwa, "Tunatangaza majina ya wauaji wakuu wa watu wa Iran: 1- Trump 2- Netanyahu."
Dakta Larijani alikuwa akirejelea vita vya siku 12 vya Marekani na Israel dhidi ya Iran mnamo Juni mwaka jana 2025, ambavyo viliua shahidi Wairani elfu moja kote nchini na kuharibu miundombinu ya raia, kijeshi, na nyuklia ya nchi hii.
Iran, katika siku chache zilizopita, imeshuhudia ghasia na vurugu kubwa za wafanya fujo na magenge ya kigaidi, wanaotumia vibaya maandamano ya wananchi kuhusu kupanda kwa gharama ya maisha.