Jenerali Qa'ani: Freedom Flotilla imewafedhehesha Wazayuni
-
Brigedia Jenerali Esmail Qa'ani,
Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) amesema katika ujumbe wake kwamba mafanikio ya msafara wa meli za misaada ya kibinadamu kwa ajili ya watu wa Ukanda wa Gaza "Global Sumud Flotilla, yanaendelea.
Brigedia Jenerali Esmail Qa'ani, kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, amesema kwamba harakati za Freedom Flotilla zimevunja kuta bandia za eti uhuru wa ustaarabu wa Magharibi, na kuongeza: "Msafara wa meli za misaada ya kibinadamu kwa ajili ya watu wa Ukanda wa Gaza "Global Sumud Flotilla" umefedhehesha ufashisti wa Kizayuni na kuirudisha Palestina katika mazingatio ya walimwengu."
Jenerali Qa'ani amesema kwamba Global Sumud Flotilla imeharakisha kasi ya kuangamizwa utawala uliofeli wa Kizayuni kuliko ilivyokuwa hapo awali.
Mapema mwezi huu askari wa Israel walivamia na kuzuia meli 22 kati ya meli 58 za misaada ya kibinadamu zilizokuwa zikisafiri katika maji ya kimataifa kuelekea Ukanda wa Gaza unaozingirwa.
Meli hizo ni sehemu ya msafara wa pili wa Global Sumud ambao katika miezi ya karibuni umekuwa ukijaribu kuvunja mzingiro wa Israel kwa kusafirisha misaada ya kibinadamu kwa Wapalestina huko Gaza. Msafara huo uliondoka katika bandari ya Barcelona, Hispania, tarehe 12 Aprili.
Shambulio la karibuni la Israel dhidi ya meli za misaada za Global Sumud Flotilla linafuatia mashambulizi mengi ya utawala huo ghasiibu ikiwa ni pamoja na uvamizi wa Aprili 26 karibu na Ugiriki ambapo wanaharakati baadaye waliripoti vitendo vya unyanyasaji wa kiingono, mashambulizi ya kimwili, na matibabu ya kudhalilisha wakiwa chini ya ulinzi wa askari wa Israel.