Kiongozi wa machafuko yaliyofadhiliwa na Marekani mwezi Januari auawa nchini Iran
-
Abbas Akbari Feizabadi amenyongwa kwa kushiriki katika mauaji ya Januari 2026
Mahakama ya Iran imetangaza kwamba mmoja wa viongozi wa makundi yenye silaha yaliyohusika na ghasia zilizofadhiliwa na madola ya kigeni mnamo Januari 2026 amenyongwa katika mji wa Nain.
Abbas Akbari Feizabadi alitambuliwa kama mmoja wa viongozi wa magenge yaliyokuwa na silaha katika machafuko ya Nain, mkoani Isfahan, ambaye alishiriki pakubwa katika mashambulizi dhidi ya ofisi ya gavana wa kaunti, vituo vya usalama, na taasisi za huduma za umma.
Nyaraka za kesi na ushahidi wa picha zinaonyesha kwamba Akbari alikuwepo mitaani akiwa na bastola aina ya Colt, aliwafyatua risasi askari usalama, na alishiriki pamoja na waandamanaji wengine kuvamia ofisi ya gavana.
Alishtakiwa kwa makosa ya kuharibu mali ya umma kwa makusudi kwa nia ya kupinga Jamhuri ya Kiislamu, kuvuruga utulivu na usalama wa umma na njama ya kutenda uhalifu dhidi ya usalama wa ndani wa nchi.
Mahakama imempata Akbari na hatia kwa mujibu wa kukiri kwake kuhusu kubeba bastola ya jeshi, kushiriki katika machafuko ya silaha mitaani na kuwafyatua risasi askari usalama - vitendo vinavyojumuisha waziwazi kubeba silaha kwa nia ya kuhatarisha maisha na kusababisha ukosefu wa usalama wa umma.
Video ya ufyatuaji risasi na ripoti ya polisi inayothibitisha kupatikana silaha nyumbani kwake vimethibitisha zaidi hatia yake.
Kwa mujibu wa Kituo cha Vyombo vya Habari cha Mahakama, jaribio la mapinduzi lililoungwa mkono na kufadhiliwa na Marekani la Januari 8-9, 2026, lilisababisha uharibifu mkubwa nchini, na maelfu ya raia wasio na hatia na askari usalama waliuawa shahidi.