Rouhani: Kila mtu ajitahidi kuleta amani na uthabiti duniani
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kila mtu anapaswa kujitahidi kuleta amani na uthabiti katika eneo na dunia nzima kwa jumla.
Rais Rouhani ameyasema hayo leo asubuhi mjini Tehran kabla ya kuondoka na kuelekea Venezuela kushiriki katika Mkutano wa Viongozi wa Harakati ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowoete NAM.
Aliongeza kuwa, hali ya hivi sasa duniani na eneo si ya kuridhisha na kuongeza kuwa kuna umuhimu wa kuwepo amani, kutoingilia masuala ya ndani ya nchi zingine, kuheshimu mamlaka ya utawala wa kitaifa na kushirikiana katika kutatua masuala ya nchi zinazo stawi na dunia nzima kwa ujumla.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliongeza kuwa, kikao cha NAM ambayo ina nchi 120 wanachama, kitajadili masuala ya amani, mshikamano na umuhimu wa kuheshimu mamlaka ya kitaifa ya nchi.
Rais Rouhani ambaye pia anatazamiwa kushiriki katika kikao cha kila mwaka cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York amesema, atabainisha mitazamo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusu masuala ya kieneo na kimataifa katika mkutano huo utakaohudhuriwa na viongozi wa nchi mbali mbali duniani.
Baada ya kuondoka Venezuela, Rais Rouhani ataelekea nchini Cuba kwa ziara rasmi kufuatia mwaliko wa rais wa nchi hiyo.