Rais Rouhani akamilisha safari yake barani Ulaya
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amerejea nchini usiku wa kuamkia leo baada ya kukamilisha safari ya siku kadhaa katika nchi za Italia na Ufaransa.
Katika safari yake ya siku mbili nchini Ufaransa Rais Rouhani alikutana na kufanya mazungumzo na Rais wa nchi hiyo na viongozi wa ngazi za juu wa serikali ya Paris ambapo pande mbili zimejadili njia za kustawisha zaidi uhusiano na kubadilishana mawazo kuhusu masuala ya kieneo na kimataifa.
Vilevile Rais Rouhani amezungumza na wakuu wa makampuni makubwa ya kiuchumi ya Ufaransa na kuhutubia wanafikra na wataalamu wa masuala ya kimataifa. Katika safari hiyo pia Tehran na Paris zimetia saini mikataba 20 ya ushirikiano katika masuala mbalimbali huku sekta binafsi za nchi hizo mbili zikisaini mikataba zaidi ya 10 ya ushirikiano. Mikataba kadhaa ya kibiashara kati ya Iran na Ufaransa pia ukiwemo mpango wa Iran kununua ndege 114 za Airbus, imesainiwa.
Kabla ya safari yake nchini Ufaransa, Rais Hassan Rouhani alitembelea Italia na kukutana na viongozi waandamizi wa nchi hiyo. Vilevile alikutana na Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis mjini Vatican. Katika mazungumzo yake ya Papa Francis, Dakta Hassan Rouhani na mwenyeji wake walisisitiza kuwa lengo la dini za mbinguni ni kueneza amani na kuepusha wanadamu na ukatili na utumiaji mabavu. Vilevile wamesisitiza udharura wa walimwengu wote kushirikiana kwa ajili ya kukomesha machungu ya mwanadamu na kusitisha vita na mapigano kote duniani.