Rais Rouhani asisitiza kuimarishwa uhusiano kati ya Iran na Malaysia
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza juu ya udharura wa kustawishwa na kuimarishwa zaidi uhusiano kati ya Iran na Malaysia.
Rais Rouhani amesema hayo leo mjini Kuala Lumpur Malaysia katika mkutano na waandishi wa habari akiwa pamoja na Waziri Mkuu wa nchi hiyo Najib Razak na kubainisha kwamba, Iran na Malaysia zimekuwa na uhusiano mzuri na wa kidugu, lakini katika miaka ya hivi karibuni kutokana na vikwazo dhidi ya taifa hili, uhusiano wa kiuchumi kati ya nchi hizo mbili umepungua.
Rais wa Iran amesisitiza kama ninavyomnukuu: "Leo katika hatua ya awali tumefikia maamuzi ya kurejesha uhusiano wetu kama ilivyokuwa katika kipindi cha kabla ya vikwazo; na katika hatua ya pili ni kuongeza uhusiano huo maradufu.
Rais Rouhani ambaye yuko nchini Malaysia kwa ziara rasmi, baada ya kufanya mazungumzo na Najib Razak, Waziri Mkuu wa Malaysia na kushiriki katika kikao cha pamoja na ujumbe wa nchi mbili amewaambia waandishi wa habari mjini Kuala Lumpur kwamba, kuwa na uhusiano na Asia ikiwemo nchi rafiki na ndugu kama Malaysia ni jambo lenye nafasi maalumu katika sera za kigeni za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Rais Rouhani amesema, miongoni mwa mambo yaliyokuwa ajenda kuu za mazungumzo kati yake na Waziri Mkuu wa Malaysia ni suala la hitilafu za kutwishwa katika Ulimwengu wa Kiislamu pamoja na tatizo la ugaidi, ambalo ni daghadagha ya pamoja ya nchi za Mashariki ya Kati na ulimwengu kwa ujumla.