Velayati: Ushindi unapatikana chini ya kivuli cha umoja
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Mwamko wa Kiislamu amesema kuwa, mahudhurio makubwa ya maulamaa wa Suni na Shia kutoka nchi mbalimbali katika Mkutano wa Mwamko wa Kiislamu uliofanyika nchini Iraq sambamba na operesheni ya kuukomboa mji wa Mosul kutoka kwenye makucha ya magaidi wa Daesh ni ujumbe mkubwa kwamba ushindi unapatikana katika kivuli cha umoja na mshikamano wa Waislamu.
Dakta Ali Akbar Velayati aliyasema hayo jana katika kikao cha kuhitimisha Mkutano wa 9 wa Baraza Kuu la Jumuiya ya Kimataifa ya Mwamko wa Kiislamu uliofanyika mjini Baghdad, Iraq na kuongeza kuwa, kushiriki kwa maulamaa na wanazuoni zaidi ya 50 wa Suni na Shia kutoka nchi 22 na kubadilishana mawazo kuhusu masuala muhimu ya ulimwengu wa Kiislamu tena nchini Iraq ni tukio zuri na lenye baraka.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Muungano wa Kitaifa wa Iraq, Sayyid Ammar Hakiim ambaye pia amehutubia sherehe za kufunga mkutano huo ameishukuru Jamhuri ya Kiislamu hususan Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei na kuitaja Iran kuwa ni miongoni mwa nchi muhimu atika ulimwengu wa Kiislamu zinazofanya jitihada kubwa za kuimarisha umoja na mshikamano baina ya Waislamu na kuwatetea watu wanaodhulumiwa.
Mkutano wa 9 wa Baraza Kuu la Jumuiya ya Kimataifa ya Mwamko wa Kiislamu uliofanyika mjini Baghdad kwa kaulimbiu ya Umoja baina ya Waislamu, kupambana na ugaidi na kutimiza malenga ya Wapalestina, ulikamilisha kazi zake jana mjini Baghdad baada ya vikao vya siku mbili.
Jumuiya ya Kimataifa ya Mwamko wa Kiislamu iliasisiwa miaka sita iliyopita kwa ubunifu wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei.