Rais Rouhani ampongeza Aoun kwa kuchaguliwa kuwa Rais mpya wa Lebanon
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i18559-rais_rouhani_ampongeza_aoun_kwa_kuchaguliwa_kuwa_rais_mpya_wa_lebanon
Rais Hassan Rouhani amempongeza Michel Aoun kwa kuchaguliwa kuwa rais mpya wa Lebanon na kueleza matumaini yake kwamba katika kipindi hiki kipya uhusiano wa Iran na Lebanon utastawishwa zaidi ya ilivyokuwa katika siku za nyuma.
(last modified 2026-03-03T12:46:59+00:00 )
Nov 01, 2016 00:05 UTC
  • Rais Rouhani ampongeza Aoun kwa kuchaguliwa kuwa Rais mpya wa Lebanon

Rais Hassan Rouhani amempongeza Michel Aoun kwa kuchaguliwa kuwa rais mpya wa Lebanon na kueleza matumaini yake kwamba katika kipindi hiki kipya uhusiano wa Iran na Lebanon utastawishwa zaidi ya ilivyokuwa katika siku za nyuma.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameyasema hayo katika mazungumzo aliyofanya kwa njia ya simu na Rais Aoun ambapo mbali na kueleza kwamba kuchaguliwa kiongozi huyo kuwa rais mpya wa Lebanon ni dhihirisho la utulivu na ushindi wa demokrasia kwa mirengo yote ya kisiasa ya nchi hiyo amesisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu iko tayari kustawisha uhusiano na nchi rafiki ya Lebanon katika nyanja zote.

Michel Aoun, Rais mpya wa Lebanon

Dakta Rouhani ameongeza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaitakidi kuwa uchaguzi huo uliofanyika katika anga huru na salama ya ushindani si ushindi kwa mrengo mahususi bali ni dhihirisho la matokeo ya kuishi kwa amani na masikilizano jamii mbalimbali katika nchi ya Lebanon na mafanikio mazuri mno kwa taifa hilo.

Sambamba na kueleza jinsi alivyofurahi kuona kwamba baada ya ombwe la uongozi la takribani miezi 30 taifa la Lebanon limeweza kukivuka kwa salama kipindi hicho kigumu, Rais Rouhani amesema, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikisistiza kila mara kwamba endapo Lebanon haitoandamwa na mashinikizo ya maajinabi, wananchi wa nchi hiyo watakuwa na uwezo wa kumchagua rais wao.

Kwa upande wake, Rais Michel Aoun amemshukuru Rais Rouhani na kueleza kwamba Lebanon daima inataka kupanua na kustawisha uhusiano na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Wabunge wa Lebanon katika mchakato wa kumchagua rais mpya

Bunge la Lebanon jana lilimchagua Michel Aoun, kiongozi wa mrengo wa mabadiliko na marekebisho kuwa rais mpya wa nchi hiyo baada ya kiti cha urais kubaki kitupu kwa zaidi ya miaka miwili kutokana na kukosekana kufikiwa mwafaka juu ya suala hilo kati ya mirengo ya kisiasa ya nchi hiyo.../