Larijani: Israel inatumia ugaidi kudhoofisha ulimwengu wa Kiislamu
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i18934-larijani_israel_inatumia_ugaidi_kudhoofisha_ulimwengu_wa_kiislamu
Spika wa Majlisi ya Ushauri wa Kiislamu, Bunge la Iran, amesema kuwa, kueneza ugaidi ni katika mbinu na sera zinazotumiwa na utawala wa Kizayuni wa Israel kuzidhoofisha nchi za Kiislamu.
(last modified 2026-02-25T03:34:48+00:00 )
Nov 06, 2016 14:28 UTC
  • Larijani: Israel inatumia ugaidi kudhoofisha ulimwengu wa Kiislamu

Spika wa Majlisi ya Ushauri wa Kiislamu, Bunge la Iran, amesema kuwa, kueneza ugaidi ni katika mbinu na sera zinazotumiwa na utawala wa Kizayuni wa Israel kuzidhoofisha nchi za Kiislamu.

Ali Larijani amesema hayo leo Jumapili hapa mjini Tehran wakati alipokutana na wabunge kadhaa kutoka Tunisia. Katika mazungumzo hayo Larijani amebainisha masikitiko yake kuhusu kuendelea mgogoro katika eneo hili na kusema:

"Kuzusha malumbano baina a madhehebu za Kiislamu ni kati ya sera zinazofuatwa na Marekani pamoja na utawala wa Kizayuni ili kuyadhoofisha mataifa ya Waislamu na kwa msingi huo nchi za Kiislamu zinapaswa kuwa waangalifu ili kuzima njama hizo."

Larijani amesisitiza kuwa, sera za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kuleta maelewano baina ya nchi za Kiislamu. Ameongeza kuwa, fikra mgando za baadhi ya nchi za Kiislamu zinazuia umoja na maelewano ya nchi za Kiislamu.

Spika wa Bunge la Iran katika mazungumzo na wabunge kutoka Tunisia, Tehran, 2016/6/11

Spika wa Bunge la Iran amesema, uhusiano wa kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni baina ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Tunisia unazidi kustawi.

Kwa upande wake, Bi. Mubaraka al Ibrahimi, kiongozi wa ujumbe huo wa wabunge wa Tunisia amesisitizia udharura wa kuimarishwa uhusiano baina ya mabunge ya Iran na Tunisia. Aidha ameikosoa vikali Saudi Arabia kwa uvamizi na mashambulizi yake nchini Yemen na mauaji yanayofanywa na ndege zake za kivita katika nchi hiyo.

Halikadhalika ameipongeza Iran kwa kuiunga mkono serikali na watu wa Syria. Mbunge huyo wa Tunisia amesema Iran ni nchi pekee ambayo inawasaidia wananchi na serikali ya Syria katika hali ngumu iliyopo hivi sasa.