Rais Rouhani: Uingiliaji wa kijeshi ni tishio kwa usalama wa dunia
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, uingiliaji wa kijeshi katika masuala ya ndani ya nchi nyingine ni tishio kubwa kwa usalama na amani ya dunia.
Rais Hassan Rouhani amesema hayo leo hapa mjini Tehran katika mazungumzo yake na Robert Dussey, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Togo na kusisitiza juu ya udharura wa kustawishwa zaidi ushirikiano wa nchi mbili katika asasi za kimataifa kwa ajili ya kutatua matatizo mbalimbali yanayoukabili ulimwengu hii leo.
Rais Rouhani amesema kuwa, hii leo amani na usalama unakabiliwa na hatari na kwamba, ugaidi na vitendo vya utumiaji mabavu ni changamoto mbili muhimu zinazoikabili jamii ya kimataifa.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amebainisha kwamba, katu ugaidi sio wenzo mzuri kwa ajili ya mataifa ya kigeni kufikia malengo yao katika Mashariki ya Kati.
Aidha amesema, misaada ya kifedha na kisilaha na hatua ya baadhi ya nchi ya kuwatumia magaidi kama wenzo wa kufikia malengo yao ni mambo ambayo yanapaswa kusitishwa mara moja na wakati huo huo, jumuiya za kimataifa zinapaswa kuchukua maamuzi ya pamoja kwa ajili ya kukabiliana na tatizo la ugaidi duniani.
Rais Rouhani amesema, nchi za Kiafrika zina nafasi muhimu kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kuongeza kuwa, Togo inaweza kutumia uwezo wa pande mbili kwa ajili ya kustawisha zaidi ushirikiano wa kibiashara na kisiasa.
kwa upande wake, Waziri wa Mashauri ya kigeni wa Togo, Robert Dussey ameeleza utayarifu wa nchi yake wa kushirikiana na Iran katika vita dhidi ya ugaidi na kuongeza kuwa, Afrika sio mali ya madola makubwa ya kikoloni bali ni mali ya watu wa bara hilo.