Iran kuimarisha uhusiano wa kijeshi na China
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema nchi hii inakaribisha kuimarishwa uhusiano na China katika nyanja zote ikiwemo sekta ya ulinzi.
Rais Rouhani aliyasema hayo jana Jumanne mjini Tehran alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Ulinzi wa China Chang Wanquan. Rais wa Iran ameongeza kuwa, ugaidi na uingiliaji haramu wa baadhi ya madola katika masuala ya ndani ya nchi zigine ni hatari na vitisho viwili vikubwa.
Rais wa Iran amebainisha jitihada za Iran katika kulinda uthabiti na usalama wa eneo sambamba na mapambano dhidi ya ugaidi na kuongeza kuwa, kunapaswa kuwepo ushirikiano zaidi wa Tehran na Beijing katika vita dhidi ya hatari kubwa ya ugaidi.
Rais Rouhani amesisitiza kuwa haiwezekani kutenganisha usalama wa bara Asia na eneo muhimu la Bahari ya Hindi, Bahari ya China na Ghuba ya Uajemi. Kwa msingi huo amesema nchi za Asia zinapaswa kushirikiana kulinda usalama wa eneo hilo na kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina nafasi muhimu sana katika kuhakikisha usalama na uthabiti unapatikana dunaini.
Kwa upande wake Cahng Wanquan, Waziri wa Ulinzi wa China ameashiria nafasi ya kistratijia ya Iran katika eneo na kusema kuna udharura wa kuimarisha uhusiano wa nchi mbili katika nyanya mbali mbali. Amesema China daima imekuwa na misimamo inayokaribiana sana na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.