Iran: Ugaidi ni tishio kwa nchi za Afrika na Asia Magharibi
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambaye anashughulikia masuala ya nchi za Kiarabu na Kiafrika amesema ugaidi ni tatizo la kimataifa na tishio la pamoja kwa nchi za bara Afrika na eneo la magharibi mwa bara Asia.
Hussein Jaber Ansari aliyesema hayo jana Jumatatu katika mazungumzo yake na Kamishna Mkuu wa Baraza la Usalama na Amani la Umoja wa Afrika, Smail Chergui aliyeko safarini hapa mjini Tehran na kuongeza kuwa, ni jambo la kusikitisha kuona baadhi ya nchi za eneo na kimataifa zinatumia ugaidi kufanikisha maslahi yao ya kisiasa.
Amesema ni kwa sababu hiyo ndio maana nchi hizo haswa za Magharibi zimeugawanya ugaidi katika sehemu mbili: Ugaidi mzuri na ugaidi mbaya na kwamba hili limechangia kutozaa matunda vita dhidi ya jinamizi hilo.
Wakati huo huo, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika masuala ya nchi za Kiarabu na Kiafrika amezungumzia suala la kuimarisha ushirikiano kati ya Iran na nchi za Afrika, akisisitiza kuwa, kuna nyanja mbali mbali za kuboresha ushirikiano kati ya Jamhuri ya Kiislamu na AU.
Awali Kamishna Mkuu wa Baraza la Usalama na Amani la Umoja wa Afrika, Smail Chergui alikutana na kufanya mazungumzo na Dakta Muhammad Javad Zarif Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikisisitiza mara kwa mara kwamba, inatoa kipaumbele katika siasa zake za kigeni juu ya suala la ushirikiano na nchi za Kiafrika.
Baada ya mkutano kati ya Chergui na Jaberi Ansari, wawili hao walisaini hati ya maelewano katika nyuga za amani na usalama, ambayo inatumiwa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Umoja wa Afrika kama msingi wa kuimarisha ushirikiano wa pande mbili.