Rais Rouhani asisitiza kuimarishwa uhusiano wa Iran na Slovenia
Rais Hassan Rouhani amesisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Slovania zimeazimia kwa dhati kustawisha uhusiano wa pande mbili katika nyanja mbalimbali zikiwemo za kiuchumi na kisiasa.
Rais wa Iran ametoa sisitizo hilo leo hapa mjini Tehran katika mkutano na waandishi wa habari aliofanya pamoja na mgeni wake Rais Borut Pahor wa Slovenia aliyeko safarini hapa nchini na kueleza kuwa mbali na uhusiano wa kiuchumi, Iran na Slovenia zinatilia mkazo kustawisha uhusiano wa kiutamaduni, kisayansi na kiteknolojia na kwamba hati zilizosainiwa katika uga wa teknolojia ya ICT na Nano zinaonyesha kuwa nchi hizo mbili zimeamua kupanua ushirikiano wao katika uga wa teknolojia mpya.
Rais Rouhani ameongeza kuwa safari ya Rais wa Slovenia hapa nchini ni ya kwanza kufanywa na rais wa nchi hiyo hapa nchini, na kufunguliwa ubalozi wa Slovenia mjini Tehran kunadhihirisha irada thabiti ya nchi mbili katika kustawisha uhusiano wao.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amebainisha kuwa Jamhuri ya Kiislamu inaupa umuhimu uhusiano wake na Umoja wa Ulaya; na safari ya Rais wa Slovenia hapa nchini ni hatua moja mbele ya kuimarisha uhusiano na Umoja wa Ulaya na kustawisha uhusiano na Slovania.
Katika mkutano huo na waandishi wa habari, Rais Borut Pahor wa Slovenia amesema safari yake hapa nchini akiwa amefuatana na ujumbe mkubwa wa kiuchumi inaashiria kuanza kufunguliwa ukurasa mpya katika uhusiano wa nchi mbili.
Rais wa Slovania amesisitiza kuwa Iran na Slovenia zina mtazamo mmoja katika masuala mengi ya kimataifa na nchi zote mbili zinaitakidi kuwa mizozo ya kieneo na kimataifa inaweza kutatuliwa kwa njia za kidiplomasia na za amani.
Rais Borut Pahor wa Slovenia aliwasili mjini Tehran jana jioni kwa safari rasmi yenye lengo la kustawisha uhusiano wa nchi yake na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.../