Rais Rouhani: Kuhuisha njia ya mashahidi ni jukumu la watu wote
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i20326-rais_rouhani_kuhuisha_njia_ya_mashahidi_ni_jukumu_la_watu_wote
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amewaenzi mashahidi wa mlipuko wa Hilla Iraq uliowalenga Mazuwwar na kusema kuwa, kuhuisha njia hii ya mashahidi na kuzisaidia familia zao ni jukumu la watu wote.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 28, 2016 00:55 UTC
  • Rais Rouhani: Kuhuisha njia ya mashahidi ni jukumu la watu wote

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amewaenzi mashahidi wa mlipuko wa Hilla Iraq uliowalenga Mazuwwar na kusema kuwa, kuhuisha njia hii ya mashahidi na kuzisaidia familia zao ni jukumu la watu wote.

Rais Rouhani amesema kuwa, vitendo vilivyo dhidi ya ubinadamu vinavyofanywa na makundi yenye kufurutu ada katika ardhi ya Iraq ambavyo vimekuwa vikiwalenga pia wafanyaziara wa mataifa mbalimbali wakiwemo wa Kiirani, kwa mara nyingine vimeimarisha azma ya taifa la Iran ya kukabiliana na magaidi na kung'oa mizizi ya fikra za ugaidi pamoja na waungaji mkono wake wa kimataifa.

Katika barua yake kwa taasisi ya mashahidi hapa Iran, Rais Rouhani ametaka mashahidi wa Kiirani wa matukio ya kigaidi ya Hilla na Kirkuk nchini Iraq wajumuishwe katika orodha ya mashahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Shambulio la kigaidi dhidi ya Mazuwwar katika mji wa Hilla Iraq

Rais Rouhani anayasema hayo siku moja tu baada ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei kutoa ujumbe maalumu kuhusiana na kuuawa shahidi wafanyaziara huko Iraq.

Wafanya ziara zaidi ya 100 waliuawa shahidi na wengine wengi kujeruhiwa siku ya Alkhamisi iliyopita, kufuatia hujuma ya trela la mafuta lililokuwa limetegwa bomu kuripuka katika kituo cha petroli cha eneo la Al Shumali katika mji wa Hilla mkoani Babol kusini mwa Baghdad, Iraq. Idadi kubwa ya wafanyaziara waliouawa shahidi katika hujuma hiyo ambayo kundi la kigaidi la Daesh lilidai kuhusika nayo, walikuwa Wairani.