Rais Hassan Rouhani: Muswada wa Bunge la Marekani ni ukiukaji wa JCPOA
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, taifa la Iran litachukua hatua madhubuti na za kivitendo mkabala na uvunjaji ahadi, kigugumizi na ucheleweshaji wa aina yoyote ile katika kutekeleza mapatano ya nyuklia yajulikanayo kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA).
Rais Hassan Rouhani amesema hayo leo katika hotuba yake kwenye Bunge la Iran na kubainisha kwamba, katu hakuna wakati Tehran itakuwa ni mkiukaji wa makubaliano ya nyuklia na kusisitiza kwamba, taifa hili litatoa jibu mwafaka kwa ukiukaji wa makubaliano ya nyuklia kwani muswada uliopasishwa hivi karibuni katika Bunge la Marekani ni ukiukaji wa wazi wa makubaliano hayo.
Rais Rouhani amebainisha kuwa, Rais wa Marekani anapaswa kutekeleza majukumu yake ipasavyo na kwa kutumia mamlaka aliyonayo azuie utekelezwaji kivitendo vikwazo vilivyoongezewa muda dhidi ya Iran.
Rais Hassan Rouhani amebainisha kwamba, Iran inatambua kuwa, suala la kupanua ushirikiano wake kimataifa ni haki yake hivyo haina haja ya kuiomba ruhusa nchi fulani kuhusiana na jambo hilo.
Hayo yanajiri katika hali ambayo, Wabunge wa Majlisi ya Ushauri wa Kiislamu (Bunge la Iran) leo nao wamelaani hatua ya wajumbe wa Bunge la Marekani kurefusha kwa muda wa miaka 10 sheria ya kuiwekea Iran vikwazo na wametoa wito wa kuchukuliwa hatua mwafaka zinazoendana na hatua hiyo ya Bunge la Marekani.
Itakumbukwa kuwa, Julai 14 mwaka jana, Iran na nchi zinazounda kundi la 5+1 zilifikia mapatano ya nyuklia yajulikanayo kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA). Baada ya mapatano hayo Bunge la Iran lilipitisha sheria maalumu ambayo inaainisha ni hatua gani zitakazochukuliwa iwapo moja kati ya madola sita makubwa duniani yatakiuka mapatano hayo.