Rais Rouhani: Jibu la Iran kwa ukiukaji wa JCPOA litakuwa kali
Rais Hassan Rouhani amesisitiza kuwa Iran haitairuhusu Marekani ikiuke au iichane hati ya makubaliano ya nyuklia yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA).
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameyasema hayo leo katika hotuba aliyotoa mbele ya hadhara ya wanachuo wa Chuo Kikuu cha Tehran katika maadhimisho ya Siku ya Wanachuo.
Akizungumzia kauli za vitisho zilizotolewa na serikali ijayo ya Marekani ya kukiuka na kuichana hati ya JCPOA, Rais Rouhani amesema Marekani haiwezi kuathiri irada, kusimama imara na muqawama wa taifa la Iran.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema Marekani inakwenda kinyume na makubaliano katika utekelezaji wa hati ya makubaliano ya nyuklia na akasisitiza kwa kusema: "Endapo vikwazo vya miaka 10 vya Marekani dhidi ya Iran vitatekelezwa na rais wa Marekani jibu la Iran litakuwa kali na linalostahiki".
Dakta Rouhani ameashiria pia njama za maadui za kueneza hofu juu ya Iran na kueleza kwamba Iran si hatari kwa nchi yoyote; bali ni Marekani na utawala wa Kizayuni ndizo hatari kwa walimwengu.
Aidha amesisitiza kuhusu uhuru wa kujitawala kisiasa taifa hili kwa kusisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaendelea na harakati yake ya kufuata njia ya maendeleo na Mapinduzi.
Sambamba na kutilia mkazo msimamo wa kukabiliana na maadui kwa ajili ya kutetea haki za wananchi wa Iran, Rais Rouhani amesema, kwa umoja na mshikamano Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itayavuka matatizo yote yakiwemo ya kiuchumi.../